Halmashauri ya Mbulu yatakiwa kutekeleza maagizo ya LAAC

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeitaka Halmshauri ya Wilaya ya Mbulu kufanyia kazi ushauri na maagizo iliyoyatoa mara baada ya kamati hiyo kufanya ukaguzi na kubaini baadhi ya changamoto katika utekelezaji wa mradi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na Shule ya Sekondari Tumati.

LAAC imetoa maelekezo hayo Machi 17, 2024 wakati ilipofanya ziara ya kukagua miradi iliyotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya Mbulu mkoani Manyara.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ester Bulaya amewaasa watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kutekeleza kikamilifu majukumu yao pindi wanapopewa dhamana ya kusimamia fedha za umma katika utekelezaji wa mradi ili ikamilike kwa wakati na ubora pamoja na kuendana na thamani ya fedha iliyotolewa.

“Hizi fedha za miradi ni za wananchi hivyo ni vema mkawa na uchungu nazo na kuzisimamia ili ziwe na tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi,” Bulaya amesisitiza.

Awali, ikisomwa taarifa ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbulu na ujenzi wa miundombinu ya kidato cha tano na cha sita ya shule ya sekondari Tumati, kamati iliitaka halmashauri hiyo kuondoa changamoto zote zilizobainiwa na kamati katika shule ya sekondari Tumati na kufuata taratibu na miongozo iliyotolewa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI.

Habari Zifananazo

Back to top button