Halmashauri zatakiwa kutenga matumizi bora ya ardhi

HALMASHAURI zimetakiwa kupanga  Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi ili kukabiliana na migogoro ya Ardhi na mipaka ya vijiji nchini

Katibu Tawala wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Pendo Ndumbaro ametoa agizo hilo jana, alipokuwa akifungua mkutano wa wadau kujadili rasimu ya Mpango wa matumizi ya ardhi uliondaliwa na mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi (LTIP) kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo.

Amesema hatua hizo ni pamoja na kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa vijiji, upimaji wa vipande vya ardhi na kutoa hatimiliki za kimila.

“Napenda kushauri kuwa Mpango huu utumike kumaliza migogoro ya matumizi ya ardhi na migogoro ya mipaka ya vijiji, Mpango huu ukawe dira ya Matumizi sahihi ya kila kipande cha ardhi ndani ya Halmashauri ya wilaya ya Mbinga.”Amesema

Amesema, pia  Mpango huo uanishe na kutoa njia sahihi za kusimamia utunzaji wa maeneo ya hifadhi za vilele vya milima, misitu na vyanzo vya maji na  kuweka maeneo ya kimkakati ya uwekezaji kutokana na rasilimali zilizopo ndani ya halmashauri ya wilaya ya Mbinga.

Aidha, amesema moja ya vipengele muhimu wakati wa utekelezaji wa mradi huo ni kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi ya halmashauri ya wilaya ambao umekwisha andaliwa rasimu na sasa ni zamu ya wadau muhimu wa maendeleo kupitia mpango huo na kutoa maoni yao.

“Pamoja na lengo hilo kuu, uandaaji wa mpango wa matumizi ya ardhi ya halmashauri ya wilaya una malengo yenye tija kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa taifa letu kama vile kufungua fursa za uwekezaji, kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi na migogoro ya mipaka, kuhifadhi mazingira na mwisho kuboresha usalama wa milki za ardhi, “amesema.

Pendo amesema,  mpango huo ni wa miaka 20 kuanzia mwaka huu 2023 hadi 2043 ukiwa na lengo kuu la kusimamia matumizi ya ardhi na kuimarisha ukuaji wa uchumi wa watu wanaoishi katika halmashauri ya wilaya kwa kuwa na matumizi endelevu ya rasilimali ardhi na kuzingatia uhifadhi wa mazingira.

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button