‘Halmashauri zitenge fedha afua za kutokomeza ukatili’

SERIKALI imeshauriwa kuona halmashauri zote nchini zinatenga asilimia mbili ya mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji afua zinazolenga kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Pia imeshauriwa wanaume kushirikishwa katika utekelezaji wa afua hizo za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Hayo yamebainishwa na Mratibu wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), Joel Mangi wakati wa kuwasilisha tathmini ya utekelezaji wa mpango huo kwenye kikao cha makatibu wakuu wa wizara zinazotekeleza afua za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Alisema katika utekelezaji wa miaka mitano wa Mpango wa Kwanza wa Mtakuwwa ambao umefikia tamati, kumekuwa na changamoto kubwa ya utengaji wa bajeti kwa ajili ya kutekeleza afua za kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.

Aidha, Mangi alisema tathmini pia imependekeza ushirikishwaji wa wanaume katika utekelezaji wa afua za kutokomeza ukatili, hatua inayoaminika itasaidia katika mapambano hayo.

“Kwa vile tafiti zinaonesha kuwa wanaume ndio wanaoongoza kutekeleza ukatili dhidi ya wanawake na watoto, hivyo imeonekana haja ya kuhakikisha wanaume nao wanashirikishwa ipasavyo katika kutekeleza afua hii. Hatua hii itasaidia kupunguza ukatili,” alisema.

Mangi alisema utekelezaji wa Mtakuwwa umewezesha uundwaji wa kamati za ulinzi wa mtoto kufikia asilimia 88.

Alisema katika kuongeza upatikanaji wa huduma rafiki kwa manusura wa ukatili ambapo mpaka sasa vituo vya mkono kwa mkono 21 vimeanzishwa, kati ya lengo la kuanzisha vituo 26 huku nyumba salama 10 zikianzishwa pia.

Mangi alisema wamefanikiwa pia kusajili wataalamu wa msaada wa kisheria wapatao 1,093 ambao wanafanya kazi kwenye mashirika 204.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x