“Halmashauri zote Mtwara ziandae mpango kukabiliana na El-Nino
NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Ummy Nderiananga amezitaka halmashauri zote mkoani Mtwara kuandaa mipango ya utekelezaji ya kuweza kukabiliana na maafa yanapotokea katika maeneo yao.
Akizungumza leo mkoani Mtwara wakati akifungua mafunzo ya siku mbili yanayoendelea mkoani humo kuhusu masuala ya maafa kwa kamati ya maafa ngazi ya mkoa kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Naibu Waziri huyo amesema awali kulikuwa ugumu wa utekelezaji wa sheria ambapo sasa imefanyiwa maboresho mwaka 2022.
Aidha maboresho hayo yamekuja kufuatia maoni yaliyotolewa na wadau mbalimbali wakiwemo wabunge wote nchini namna ya kufanya ili sheria hiyo iweze kufanya kazi vizuri.
Amesema kwa mujibu wa sheria ya usimamizi wa maafa namba 6 ya mwaka 2022 na kanuni zake imeanzisha kamati za usimamizi wa maafa za mikoa, wilaya, kata, vijiji au mitaa ambapo jukumu la msingi la kamati hiyo ni kuchukua hatua kwa lengo la kuzuia, kupunguza madhara ya majanga ya aina mbalimbali ikiwemo mafuriko.
‘’Mjipange mapema kila mmoja katika eneo lake aweze kuchukua hatua pia kushirikisha wadau na wananchi kwa ujumla katika suala hili ili kima mmoja aone kuwa maafa ni jambo la kila mtu na siyo la mtu mmoja pekee’’amesema Nderiananga
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas amesema anafarijika na kitu hicho kinachofanyika kwa wajumbe hao ambapo ni matayarisho kutokana na taadhari waliyoipata ya uwepo kwa mvua za El-Nino.
Amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo wajumbe katika kupunguza athari ya maafa hatua kwa hatua kupitia juhudi mbalimbali za kuainisha na kusimamia vyanzo visababishi vya maafa ikiwa ni pamoja na kupunguza uwezekano wa kuathariwa au kuzuiliwa watu na mali zao.