DAR ES SALAAM: MWENYEKITI wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania, Sheikh Alhad Mussa Salum amewataka Waumini wa dini ya Kiislam nchini kote kuendeleza mambo mema waliyoyafanya kipindi cha mwezi mtukufu wa ramadhani.
Sheikh Mussa amesema kutekeleza ibada ya mfungo wa ramadhani ni bahati inayotakiwa kumshukuru Mungu kwa ibada ya kuendeleza mambo mema yote yaliyokuwa yakifanywa kipindi cha mfungo huo.
Amesema katika sikukuu ya Iddi waumini wa kiislam wanatakiwa kutembelea yatima, wajane na watu wenye uhitaji maalum ili wafurahi nao pamoja kwa kuwapa vyakula tena hasa vyakula pendwa wakati wa sikukuu ikiwemo mchele (pilau) na vinginevyo.
“Siku ya Iddi ni siku tukufu sana Mungu ameriidhia, hii ni sikukuu ya moja kwa moja Muumini wa kiislam anatakiwa akumbuke utukufu wa siku hii, kila muislam anatakiwa atembelea yatima, wajane na wote wenye uhitaji wapate furaha ambayo walitamani kuipata lakini kutokana na mazingira yao wanashindwa pia siku hii ni siku ya kusameheana nakuendeleza undugu,” amesema Alhad.
Pia Sheikh Alhad Mussa amewataka wazazi wawapeleke watoto wao katika maeneo yanayofaa kusherehekea sikukuu hiyo na si vinginevyo.
“Wazazi wanatakiwa kuwa makini na watoto wao wasiwachanganye katika magari yanayokwenda kwenye fukwe watoto wa kike na kiume hawatakiwei kuchanganywa kwenye magari hayo ni upotofu wa maadili ya muislam na pia tusherehekeee sikukuu ya Iddi bila kuvuka mipaka ya Mungu,” amesema.