Hatma ya Saitoti kujulikana kesho

HATMA ya Madini ya Tanzanite kilo 4 yenye thamani ya mamilioni ya pesa yanayodaiwa kuchimbwa katika mgodi wa Kitalu C katika Mji wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara na mfanyabiashara, Joel Mollel maarufu kwa jina la Saitoti itajulikana kesho Machi 24, 2023.

Saitoti anayemiliki Kampuni ya Gem & Rock Venture ya Jijini Arusha anachimba madini ya Tanzanite katika Kitalu B anatuhumiwa kuchimba kinyemela{Bomu} katika Mgodi wa Kitalu C na kufanikiwa kupora madini kiasi hicho mbali ya kuonywa kwa maandishi zaidi ya mara mbili na Wizara ya Madini kuacha kuchimba katika mgodi lakini alikaidi.

Afisa Mfawidhi wa Wizara ya Madini Mkoa wa Manyara ,Mernad Msengi alisema timu ya Wataalamu wa ramani mgodini kutoka Chuo Cha Madini Mkoani Dodoma imeshafika na imeshaanza kazi toka march 20 mwaka huu na ndani siku zisizozidi sita taarifa rasmi ya madini ya Kilo 4 itakuwa tayari kama madini hayo ni ya kitalu C au la.

Advertisement

Msengi alisema timu hiyo ya Wataalamu inafanya kazi kwa muda wote ndani ya mgodi kushirikiana na vyombo vyote vya dola katika Wilaya ya Simanjiro{Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Simanjiro}, Viongozi wa Mgodi wa Kitalu C na B na baadhi ya Maofisa wa Wizara ya Madini lengo ni kutaka taarifa za kiuchunguzi ziwe wazi na zisiwe na kificho ili kuondoa lawama zisizokuwa za Msingi kwa pande zote.

Alisema baada ya yeye kukabidhiwa taarifa za kiuchunguzi atatoa taarifa rasmi kwa vyomo vya habari na hatua gani zitachukuliwa itajulikana siku hiyo kwani kila kitu kipo kwa mujibu wa sheria na sio vinginevyo.

‘’Timu ya Wataalamu wa ramani za madini Migodini imewasili Mirerani na tayari imeanza kazi rasmi na itafanya kazi kwa muda usiozidi siku sita na baada ya hapo taarifa itatolewa rasmi ‘’ alisema Msengi

Saitoti anayemiliki Kampuni ya Gem & Rock Venture kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mwenza,Sammy Mollel katika Mgodi Kitalu B wanatuhumiwa kuchimba Bomu katika Mgodi wa Kitalu C mgodi unamilikiwa na serikali na Mwekezaji Mzawa Onesmo Mbise maarufu kwa jina la Onee na kufanikiwa kutoweka na madini kilo 4 lakini kabla ya kukimbia nayo  Maofisa wa Wizara ya Madini Mirerani walifanikiwa kuwapora na kuyahifadhi katika ofisi Madini Mirerani.

Rais Dk Samia Suluhu Hassan aliwahi kusema katika hotuba zake siku za nyuma kuwa wale wote wanaochimba Bomu katika mgodi wa Tanzanite Kitalu C kuacha mara moja vinginevyo dola haitawaacha salama pindi watakapokaidi amri kwani kitalu C ni mali ya serikali na Mwekezaji Mzawa anayemiliki Kampuni ya Uchimbaji ya Franone ya Jijini Arusha.

Hata hivyo kwa mujibu wa sheria ya madini ikibainika kuwa madini hayo yalichimbwa kitalu C kuna hatua nyingi zitachukuliwa dhidi ya wahusika ikiwemo kufunguliwa mashitaka ya Uhujumu Uchumi.

Hivi karibuni ilidaiwa kuwa wafanyakazi 30 wa Kampuni ya Gem & Rock Venture walivamia mgodi wa Kitalu C kwa njia ya Bomu na kuchimba Madini ya Tanzanite kibabe ndani ya mgodi huo na kufanikiwa kupora Madini ya kilo 4 hayo lakini uongozi wa Kampuni Ya Saitoti  ulipinga na kusema kuwa wao ndio wameporwa Madini ya Tanzanite yenye uzito wa kilo 6.