Hatma ya Simba, mikononi mwa Geita Gold FC

Hatma ya wanaoshuka kufahamika kesho

DAR ES SALAAM: WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara inafikia tamati kesho, hatma ya Simba SC kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao ipo mikononi mwa Geita Gold FC katika mchezo dhidi ya Azam FC.

Simba kesho wanashuka dimbani kuvaana na JKT Tanzania uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam. Inahitaji kushinda mchezo huo ili kujihakikishia nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL).

Azam FC wapo nafasi ya pili wakiwa na alama 66 sawa na Simba ambao wanashika nafasi ya tatu na kila mmoja anahitaji ushindi katika mchezo wa kesho.

Upande wa mabingwa wapya wa msimu na mara tatu mutawalia, Yanga SC watashuka dimbani kesho kwaajili ya kukamilisha ratiba, dhidi ya Tanzania Prisons, Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, ilhali Simba watawakaribisha JKT Tanzania Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.

Mitanange mingine, Geita Gold FC wakiwa nyumbani Uwanja wa Nyankumbu kuikaribisha Azam FC. Namungo FC dhidi ya Tabora United, katika dimba la Majaliwa mkoani Lindi. Singida Fountain Gate FC dhidi ya Kagera Sugar, Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Coastal Union ‘Wana Mangushi’ dhidi ya KMC FC, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Mashujaa FC watakuwa nyumbani kuikaribisha Dodoma jiji FC, Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma na  Ihefu FC dhidi ya Mtibwa Sugar ambao tayari imeshuka daraja.

Katika michezo hiyo, kuna vita ya kuwania nafasi ya pili lakini vita vikali ipo katika kuwania tuzo ya ufungaji bora kati ya viungo washambuliaji wawili Stephen Aziz Ki wa Yanga na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wote wakiwa wamefunga mbaoa 18.

SOMA: Mechi tatu za maamuzi, vita ya Ligi Kuu

Kuna timu ambazo zinajinasua kushuka na kutafuta nafasi ya kucheza hatua ya mtoano ‘Play Off’ ambapo Geita Gold FC iliyo nafasi ya 15 ya pili kutoka chini itavaana na Azam FC ambayo nayo ipo katika vita vya kutafuta nafasi ya pili ili kucheza CAFCL msimu ujao.

Matumaini ya Simba kucheza CAFCL msimu ujao yamebebwa na Geita Gold FC ambayo ikimfunga Azam FC, inaenda kucheza Play Off na kuipa mwanya Wekundu wa Msimbazi kwenda kucheza michuano ya ligi ya Mabingwa.

 

Kuelekea mchezo huo, Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda amesema maandalizi ya mchezo wa kesho upo vizuri na muhimu kwao kupata matokeo ya ushindi.

“Naweza kesho ndio tunafunga shule kwa sababu tunamaliza mechi ya mwisho wa kumaliza ligi ni muhimu kwetu kushinda na kufikia malengo yetu, mechi hii ni ya maamuzi na kila mmoja ana mahitaji yake. Itakuwa mechi inamahiyaji maluea na dakika 90 tutapata maamuzi.

Licha ya kufanya vizuri lakini wachezaji wangu wapo vizuri kisaikolojia na wanafahamu umuhimu wa kushinda mchezo wa leo,” amesema Mgunda.

KOCHA Msaidizi wa Simba, Juma Mgunda

Kocha Msaidizi wa JKT Tanzania, George Mketo amesema wamejianda kwa mchezo wa kesho, wanaimani utakuwa mchezo mgumu kulingana na mahitaji ya kila timu kwa upande wao kupata matokeo mazuri.

Amesema wanafahamu ubora wa Simba hasa katika maeneo ya pembeni na kati, hivyo wanaenda kupambana kutafuta matokeo chanya na kupata alama.

“Simba ina wachezaji wakubwa na wakomavu na tunaenda kucheza kwa namna mbili kukabilian na ubora wa wapinzani wetu na kufanikiwa kuvuna alama muhimu ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kusalia katika ligi,” amesema Mketo.

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema wachezaji wake wapo vizuri na wapo tayari kwa mchezo huo, na kuongeza kuwa  watacheza kwa tahadhari kubwa kwa sababu ya ubora wa mpinzani wao.

Amesema hakuna siri yoyote zaidi ya wachezaji kupambana na mashabiki wao kuwaunga mkono katika kila hali na anaimani ya kufanya vizuri katika michezo miwili iliyosalia leo dhidi ya Tanzania Prisons na fainali ya kombe la Shirikisho la CRBD Bank dhidi ya Azam FC.

“Tumefanya maandalizi mazuri kuelekea mchezo wetu dhidi ya Tanzania Prisons, wachezaji wanatambua tunahitaji nini katika mchezo wetu wa leo, kuna baadhi ya nyota nitawakosa akiwemo Jonas Mkude,” amesema kocha huyo.

Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Ahmad Ally amesema wanafahamu wanakutana na timu bora. Wamefanikiwa kuwaona Yanga walipocheza na Tabora United kwa kuona ubora wao.

“Ili uwe bora lazima ukumfunge aliyekuwa bora, ninawaheshimu na kuwapa nafasi wao na kucheza mpira kwa umakini na kuwapa presha, tunajua uhitaji wa hii mechi na sasa ligi imekuwa mgumu hasa nani anayecheza play off.

Ukiamgalia msimamo unaona hakuna mwenye uhakika wa kubaki ligi kulimgana na mtu anayeshika nafasi ya tano anaweza kuporomoka hadi chini asipokuwa makini katika mchezo huu wa leo, tunahitaji kupambana kutafuta matokeo mazuri,” amesema Ahmad.

Habari Zifananazo

Back to top button