Heri ya siku ya kuzaliwa Rais Samia

Rais Samia.

RAIS Samia Suluhu Hassan leo anatimiza umri wa miaka 63.

Alizaliwa Januari 27, 1960 katika Kijiji cha Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, baba yake alikuwa mwalimu na mama yake alikuwa mama wa nyumbani.

Machi 19, 2021 aliapishwa kuwa Rais wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama.

Advertisement

Aliapishwa baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk John Magufuli. Dk Magufuli aliaga dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam.

Kabla ya kiapo hicho Ikulu jijini Dar es Salaam, Samia alikuwa Makamu wa Rais wa Tanzania katika Serikali ya Awamu ya Tano akiwa ni mwanamke wa kwanza nchini kushika madaraka hayo.

Samia Suluhu Hassan ni Rais wa sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

 

Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM.

Kwa mujibu wa tovuti rasmi ya Rais, Samia aliingia katika siasa akiwa mwanachama wa CCM, Juni 10, 1987.

Aliingia katika siasa za uchaguzi mwaka 2000 katika nafasi ya Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Zanzibar kama Mwakilishi wa Viti Maalumu vya Wanawake hadi mwaka 2010.

Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, aligombea na kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwakilisha Jimbo la Makunduchi, Zanzibar.

Samia alipata elimu ya msingi katika shule mbalimbali ikiwemo Shule ya Msingi Chwaka iliyoko Unguja kuanzia 1966 hadi 1968, Shule ya Msingi Ziwani mwaka 1970 na Shule ya Msingi Mahonda mwaka 1972.

Baada ya hapo, alijiunga na Shule ya Sekondari ya Ng’ambo kwa ajili ya masomo ya kidato cha kwanza hadi cha tatu na Shule ya Sekondari Lumumba kwa ajili ya kidato cha nne kati ya mwaka 1973 hadi 1976.

Mwaka 1983, alipata Astashahada katika mafunzo ya takwimu kutoka Chuo cha Uchumi, Zanzibar.

Baada ya kufanya kazi kwa kipindi kifupi kwenye Wizara ya Mipango na Maendeleo, mwaka 1983 hadi 1986, alijiunga na Chuo cha Maendeleo ya Uongozi Mzumbe (IDM) kwa ajili ya masomo ya juu katika Utawala wa Umma.

Rais Samia

Aidha, alipata mafunzo mbalimbali katika taasisi ya Chuo cha Utawala wa Umma Lahore, Pakistan 1987, Taasisi ya Eastern and Southern African Management Institute (ESAMI) 1991, na Taasisi ya Uongozi ya Hyderabad India 1998 kwa ajili ya Astashahada ya Utawala.

Baada ya hapo, alijiunga na Chuo Kikuu cha Manchester kilichopo Uingereza kwa ajili ya masomo ya juu ya uchumi.

Vilevile, alipata Shahada ya Uzamili ya Maendeleo ya Jamii kupitia programu ya pamoja kati ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo Kikuu cha Southern New Hampshire, Marekani.

Mbali na uongozi, Rais Samia ni mke wa Hafidh Ameir na wamejaliwa watoto wanne wakiwamo watatu wa kiume.

/* */