Historia ya Mchinjita mpaka kuwa M/Mwenyekiti Bara ACT

KUZALIWA

Isihaka Rashid Mchinjita amezaliwa  Januari 9, 1983  katika Hospitali ya Nyangao iliyopo Wilaya ya Lindi Mkoa wa Lindi.

ELIMU YA MCHINJITA

Mchinjita alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Mahiwa iliyopo Kata ya Nyangao Halmashauri ya Mtama Mkoa wa Lindi kuanzia 1992 mpaka mwaka 1998.

Mwaka 1999 alijiunga na elimu ya sekondari katika shule ya sekondari ya wavulana Chidya iliyopo Masasi mkoani Mtwara.

Mwaka 2003 aliendelea na masomo ya sekondari ya kidato cha tano katika shule ya sekondari ya wavulana Tosamaganga iliyopo Mkoa wa Iringa akichukua masomo ya fizikia, baiologia na kemia.

Mwaka 2005 alihitimu kidato cha sita akipata ufaulu wa daraja la pili ‘division two’.

Mchinjita alikuwa na nafasi ya kusoma shahada ya udaktari wa binadamu nchini Uturuki na usimamizi wa biashara katika Chuo Kikuu cha Tumaini na State University of Zanzibar, lakini kote alikacha.

Mchinjita alijiunga na masomo ya stashahada ya ualimu katika Chuo cha Ualimu Alharamain katika kile anachokieleza kuwa ni hamu yake ya kushiriki katika kutatua changamoto ya elimu nchini huku akianika kuwa alikosa nafasi hiyo katika Chuo Kikuu Dar es salaam.

Mchinjita anasema sababu ni kuwa katika mwaka huo udahili ulifanyika kwa wanafunzi waliomaliza masomo ya kidato cha sita mwaka 2004 na wao wa mwaka 2005 ambapo kwa mara ya kwanza walifanya mtihani mwezi Februari badala ya mwezi Mei.

Anasema sera ya mikopo kwa wanafunzi hakuiunga mkono na hivyo aliamua kwenda kusoma stashahada ya ualimu kwa gharama zake.

Aidha Mchinjita anasema baada ya kuanza masomo chuoni hapo alishiriki kuanzisha shule mbalimbali za sekondari na msingi akieleza kuwa alianza kufanya hivyo kwa shule za msingi na sekondari za Ilala Islamic zilizopo Dar es Salaam.

Safari hiyo ilimuwezesha kushiriki uanzishwaji na uendelezaji wa shule zaidi ya 50 nchini huku akiainisha kuwa kwa sasa bado anaendelea na wajibu huo akiwa mkurugenzi wa shule Kilwa Islamic, Muzidalifah na Norget Memorial Secondary School iliyopo Masasi mkoani Mtwara.

Safari ya elimu ya Mchinjita iliendelea katika Chuo Kikuu Huria nchini alipojipatia mafunzo ya shahada ya sheria ( LLB).

USHIRIKI KATIKA SIASA

Historia yake ya kisiasa imeanza akiwa Shule ya Msingi Mahiwa ambapo anasema mwaka 1995  yeye alikuwa shabiki wa NCCR Mageuzi iliyokuwa chini ya Agoustino Lyatonga Mrema.

Ushabiki huo ulimfanya aonywe na mwalimu wake anayemtaja kwa jina la Mapondela ambaye ni mama mzazi wa mwanasiasa huyo huku akieleza kuwa alimtahadharisha kwa kuwa waalimu wenzake wanamueleza mwanaye anapotea.

Akiwa sekondari ya Chidya Mchinjita alijiunga na chama cha wananchi CUF ampapo aliratibu ugawaji wa kadi za CUF na JUVI CUF.

Mwaka 2013  Mchinjita alianza kushiriki harakati  za kisiasa kwa muda mwingi jimbo la Mtama Lindi ambapo wakati huo mbunge wa jimbo hilo alikuwa ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, hayati Benard Membe.

Alifanikiwa kuliingiza jimbo hilo katika uhai wa siasa za upinzani ambapo mwaka 2014 alifanikisha kupata vijiji 21 kuongozwa na CUF kutoka kwenye rekodi ya kuwa na kijiji kimoja.

Akiwa Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi  Wilaya ya Lindi Mchinjita anaeleza kufanikisha kusimamisha wagombea wa udiwani kata zote 31 za wilaya hiyo na wagombea ubunge majimbo yote mawili ya Mtama na Mchinga ambapo walifanikiwa kushinda jimbo la Mchinga na kushinda kata 13  huku akikiri kuwa kutoelewana miongoni kwa wagombea wa Ukawa kukamrahisishia kazi Nape Nnauye ambaye alishindana naye akiwa mgombea wa CUF jimbo la Mtama.

Mwaka 2019 Mchinjita alijiunga na chama cha ACT Wazalendo baada ya mgogoro uliodumu kwa miaka mitatu ndani ya chama cha wananchi CUF na mahakama kumtambua Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti.

Kuingia kwake ACT Wazalendo ni kama kuliifungua safari yake ya kisiasa na kuchukua wajibu mkubwa  zaidi. Inaelezwa kuwa kuwepo bungeni kwa wanasiasa nguli walioakisi siasa za upinzani Kusini kama Suleiman Bungara- ‘bwege’, Hamidu Bobali, Katani kulimfanya aongoze shushatanga kwa mikoa ya Lindi na Mtwara.

Alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Lindi mwaka 2019. Na baadaye Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho mwaka 2020.

Mwaka 2022 aliteuliwa kuwa Waziri Kivuli wa Nishati nafasi aliyoitumikia mpaka Februari 5, 2024.

FOMU KUGOMBEA M/MWENYEKITI BARA

Februari 16, 2024 alichukua fomu kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara wa chama hicho katika uchaguzi uliofanyika Machi 5, 2024.

Mchinjita anasema la kugombea nafasi hiyo ni kuimarisha ngome za chama hicho ili kuzifanya kuwa nyenzo muhimu ya kuwaunganisha wa Tanzania kupigania haki na ustawi wa taifa.

“Ni maoni yangu kuwa imani yangu isiyo na shaka katika harakati za kupigania demokrasia yenye kujenga taifa la wote kwa maslahi ya wote huu ni wakati sahihi kwangu kushiriki kikamilifu katika uongozi wa harakati hizi muhimu kwa taifa letu,”anasema Mchinjita Mchinjita.

Mchinjita anaeleza kuwa shauku yake ni kuimarisha sera na mwenendo wa chama hicho ili kibaki kuwa chama kinachosimama kama chama kiongozi kwenye kusukuma na kushinikiza utekelezaji wa agenda zenye maslahi kwa wananchi.

“Ni tamaa yangu kukijengea chama changu uwezo wa kuendelea kuwa chama chenye kuibua masuala na kuonesha masuluhisho ili hatimaye wananchi wakiamini na kukiwezesha kuunda serikali,” anaongeza.

MAAMUZI KUGOMBEA UMAKAMU MWENYEKITI

Mchinjita anasema uamuzi wake wa kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara ilitokana na ushauri kutoka kwa wanachama na viongozi wenzake.

“Swali gumu kulijibu kwangu ilikuwa ni kwa vipi ningeacha wajibu wa uenyekiti wa Mkoa wa Lindi. Sehemu kubwa ya wanachama na viongozi wengine wa mkoa walikuwa na wasiwasi kuwa kitendo cha kutoendelea kuwa mwenyekiti wa ACT Lindi kingezorotesha maendeleo ya chama,”

“Hisia zilikuwa kali kiasi wengine walianza kulaumu viongozi wa juu wakiwatuhumu kuwa wao wananitaka niende taifa bila kujali athari itakayotokea. Hata hivyo ujio wa Hamidu Bobali kama mtu aliyekuwa tayari kunipokea usukani ulipunguza taharuki,” Mchinjita anaiambia HabariLEO.

ANASHINDA MAKAMU MWENYEKITI BARA

Machi 6, 2024 Mchinjita anaiambia HabariLEO kuwa Mkutano Mkuu wa ACT Wazalendo umemchagua kuwa Makamu Mwenyekiti Bara wa chama hicho kwa kupata kura 517 sawa na asilimia 96.1.

Baada ya ushindi huo, Mchinjita anawaahidi Watanzania kuwa wategemee kuiona ACT  inayosimamia maslahi ya umma kwa kujenga hoja na kutoa suluhisho la kila changamoto.

“Wategemee chama imara cha siasa kitakachobeba agenda za Watanzania kwenye mjadala wa kitaifa. Tunakwenda kuifanya siasa ya nchi yetu iwatumikie wananchi na uhusiano wa maisha ya watu na siasa zetu kujengewa daraja la kutuvusha toka hapa tulipo,” anasema Mchinjita.

MALENGO BAADA YA USHINDI

HabariLEO inahoji ni wapi kwenye mashimo ambayo mtangulizi wake alishindwa kufukia anakwenda kushughulika nayo?

Mchinjita anajibu kuwa uongozi wa kisiasa na kidemokrasia ni mbio za kupokezana vijiti hivyo mtangulizi wake ametimiza wajibu wake.

“Kama kuna eneo ninalitazama kuwa ni kipaumbele cha kupigania basi ni ujenzi wa misingi imara ya kitaasisi. Chama chetu kimekuwa kwa kasi ndani ya muda mfupi. Ukuaji wa namna hii huleta changamoto za kiutawala na nidhamu ndani ya taasisi,” anasema Mchinjita.

Kiongozi huyo anasema anaamini ujenzi wa mfumo imara wa kitaasisi hukiahakikishia chama kudumu na kushinda vikwazo vingi. Ili kufikia azma hii mafunzo ya kutosha kwa viongozi na watendaji wetu ni muhimu sana. Ninakwenda kusukuma ajenda ya kuhakikisha kuwa viongozi na watendaji wetu wanapata mafunzo ya kutosha kuwawezesha kutimiza wajibu wao,” anaongeza Mchinjita.

NJIA ZA KUIJENGA ACT WAZALENDO

Mchijina anasema nafasi ya Makamu Mwenyekiti inampa wajibu wa kuwa msaidizi wa mwenyekiti katika majukumu ya kukijenga chama chetu pamoja na majukumu mahususi yanayotajwa kwenye ibara ya 86 (3) ya katiba ya ACT.

Anasema alipochukua fomu alitangaza vipaumbele vitano ambavyo ni, kuimarisha chama katika ngazi ya msingi, kupigania demokrasia ya kweli nchini, kuimarisha ngome za chama, kujenga misingi imara ya kitaasisi na kuendelea kukifanya chama cha masuala huku wakijenga nguvu ya kushinikiza utekelezaji wa masuala yenye maslahi kwa wananchi wote.

“Njia bora ya kufikia azma hii ni kuwa na uongozi wa pamoja shirikishi na wenye kupigania matokeo huku ukijiepusha na kutafuta visingizio, nitawasimamia wenzangu kupigania matokeo kwa kuwaonesha mfano badala ya masimulizi,” anaeleza Mchinjita.

CHANGAMOTO MIPANGO KUJENGA CHAMA

Makamu Mwenyekiti huyo anasema changamoto kubwa itakuwa ni kuleta ubunifu utakaowezesha chama kuwa hai katika ngazi zake zote.

“Tunahitaji kuwa na chama kinachoishi na si mfu katika kila ngazi ya uwajibikaji. Mwenzangu aliyetangulia ameacha muundo wa chama ulio kamili kuanzia matawi mpaka taifa,” anasema Mchinjita.

Anasema wajibu mkubwa ni kuhakikisha kila penye tawi la ACT Wazalendo linakuwa hai na kushiriki shughuli za ujenzi na uimarishaji wa chama.

“Ninao wajibu wa kukuza morali ya wanachama na viongozi kukitumikia chama chao kwa kupigania matokea,” anaongeza kiongozi huyo.

Habari Zifananazo

Back to top button