Hitilafu yakwamisha maelfu uwanja wa ndege

UINGEREZA – Maelfu ya wasafiri wamekwama katika viwanja vya ndege huko Uingereza kutokana na hitilafu ya mfumo wa kielektroniki wa pasipoti kuathiri nchi nzima na hivyo kuwalazimu ma afisa waangalizi wa mipaka kufanya majukumu yao kwa mikono.

Hitilafu hiyo ya mageti ya kielektroniki ilianza jana jioni na haikutatuliwa hadi saa 2 asubuhi na kusababisha abiria kukwama katika foleni ndefu za mageti ya kuwasili. Watoto walionekana kuwa wamechoka, walibaki bila chakula au maji kwa saa kadhaa katika viwanja hivyo.

Picha kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha foleni kubwa mbele ya lango la Heathrow, Gatwick, Stansted, Luton, Edinburgh na Manchester huku maelfu wakisubiri pasipoti zao kukaguliwa.

Tukio hilo kubwa linaonekana kusababishwa na kanzidata ya usalama ya Kikosi cha Mipaka iitwayo ‘Border Crossing’ ambayo ilianzishwa miaka mitatu iliyopita na kugharimu pauni milioni 372.

Mara tu baada ya saa 2.10 asubuhi Ofisi ya Mambo ya Ndani ilisema hitilafu imerekebishwa katika mfumo huo na haikuwa na ushahidi kwamba kukatika kwake kulisababishwa na shambulio la kimtandao.

 

Habari Zifananazo

Back to top button