Hoja 22 Muungano zapatiwa ufumbuzi

DODOMA; WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dk. Selemani Jafo, amesema tangu kuanzishwa kwa utaratibu wa vikao vya pamoja mwaka 2006 hadi sasa, kasi ya utatuzi wa changamoto za Muungano  imeongezeka, ambapo hoja 22 zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 25 zilizoibuliwa.

Katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024 pekee, hoja 15 zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 18 zilizokuwepo kwa kipindi hicho.

Waziri Jafo ameyasema hayo leo Machi 26, 2024 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu mafanikio ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Advertisement

Miongoni mwa miradi na programu zilizotekelezwa na kukamilika katika pande mbili za Muungano ni pamoja na miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF awamu ya I hadi III; Programu ya Usimamizi wa Bahari na Pwani (MACEMP) na Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDP).

Programu zingine ni, Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo na Sekta ya Mifugo (ASDP  L); Programu ya Kuwezesha Sekta ya Kilimo (ASSP); Programu ya Changamoto za Milenia (MCA  T); Mradi Shirikishi wa Programu za Maendeleo ya Kilimo (PADEP); na Mradi wa Udhibiti wa Uvuvi na Maendeleo Shirikishi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFISH).

Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani ya Mazao na uboreshaji wa huduma za Fedha Vijijini (MIVARF); Mradi wa Kuongeza Tija na Uzalishaji wa Zao la Mpunga (ERPP); Mradi wa Kujenga Uwezo wa Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi katika Maeneo ya Pwani (LDCF); na Mradi wa Kurejesha Ardhi Iliyoharibika na Kuongeza Uhakika na Usalama wa Chakula katika Maeneo Kame ya Tanzania.

Programu na miradi inayoendelea kutekelezwa pande mbili za Muungano ni pamoja na: miradi ya Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo (CDCF); Mradi wa Ujenzi wa Kingo za Kuzuia Maji ya Bahari; na Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia ya Vijijini (EBARR).