WANANCHI wa Zambia, Alhamisi ya Agosti 12 walifanya Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini humo imemtangaza Hakainde Hichilema kuwa mshindi katika uchaguzi wa Rais, akimuangusha Rais wa sasa, Edgar Lungu.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Zambia, Esau Chulu alitangaza matokeo rasmi ya uchaguzi huo kwa nafasi ya urais jana baada ya kupatikana hesabu za majimbo yote isipokuwa moja tu.
Hesabu hizo zimeonyesha Hichilema wa chama cha United Party for National Development (UPND) amepata kura 2,810,777 akimpita kwa mbali Rais Lungu kutoka chama cha Patriotic Front (PF) aliyepata kura 1,814,201.
Katika uchaguzi huo, wapiga kura milioni saba walikuwa wamejiandikisha kupiga kura katika nchi hiyo yenye idadi ya watu wanaokadiriwa kufikia milioni 19.
Pamoja na Rais Lungu kulalamikia baadhi ya mambo katika uchaguzi huo, lakini ametangaza kukubali matokeo na kumpongeza Rais mteule, Hichilema kwa ushindi huo.
Tunachukua fursa hii kuwapongeza wananchi wa Zambia ambao ni majirani zetu kwa kufanikisha uchaguzi huo uliomalizika kwa amani bila kuleta machafuko kama ambavyo imekuwa ikitokea katika mataifa mengine baada ya uchaguzi.
Aidha, tunampongeza Rais mteule, Hichilema kwa kuchaguliwa na wananchi kuongoza taifa hilo.
Pia tunampongeza Rais Lungu kwa kukubali matokeo kwani kitendo hicho kimeonesha uungwana na ukomavu wa kisiasa na kimetoa taswira nzuri kuwa mataifa ya Afrika yanaweza kufanya chaguzi kwa amani na mshindi kupatikana bila kuvurugana.
Hata hivyo, tunawasihi wananchi wa Zambia, baada ya kumaliza uchaguzi waendelee kushikamana na kudumisha amani, pamoja na kushiriki katika ujenzi wa taifa lao ili waweze kupiga hatu zaidi za maendeleo kwani kuna maisha baada ya uchaguzi.
Tunawasihi watangulize maslahi ya nchi kwa kuwa wao ni wamoja, wa taifa moja hivyo waungane kwa maslahi ya nchi yao ili isonge mbele bila ya vurugu au mivutano ya kisiasa isiyo na tija.
Wazambia watambue amani na utulivu ni nyenzo muhimu ya taifa lolote linalotaka kupiga hatua za maenedeleo kwani wananchi watajishughulisha na shughuli za uzalishaji mali na ujenzi wa taifa bila hofu, huku serikali ikitimiza wajibu wake wa kuwahudumia bila ya vikwazo.
Hongera wananchi wa Zambia kwa kufanisha uchaguzi mkuu kwa amani na tunawatakia kila heri katika ujenzi wa taifa lenu.