HOSPITALI moja nchini Afrika Kusini inachunguzwa kwa tuhuma za tukio la watoto wachanga kuwekwa kwenye maboksi badala ya kiangulio ‘incubator’ au vitanda katika jimbo la Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo.
Chapisho katika mtandao wa Facebook ulionyesha sehemu ya watoto wachanga katika hospitali ya jimbo la Mahikeng, wakiwa wamevikwa blanketi za hospitali za rangi ya zambarau na mirija ya kulishia chakula na kuwekwa kwenye maboksi ya kahawia, vyombo vya habari vya ndani vilisema.
Mkuu wa Afya Kaskazini Magharibi Madoda Sambatha, alisema wanachunguza suala hilo ili kubaini ni muda gani watoto hao walikaa kwenye maboksi hayo.
Sambatha aliomba radhi na kutaka utulivu wakati suala hilo likichunguzwa.
Alisema, kutokana na dharura, utaratibu unafanywa ili vitanda vya ziada vipelekwe hospitalini.
Meneja muuguzi wa hospitali hiyo ameripotiwa kusimamishwa kazi.
Waziri wa Afya Joe Phaahla mnamo Jumatatu amelielezea tukio hilo kuwa ni usimamizi duni wa wale wanaosimamia kituo hicho.