SERIKALI inatarajia kujenga hospitali kubwa yenye hadhi ya hospitali ya Mloganzila, mkoani Kagera.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu jana katika kikao chake na wataalamu wa afya mkoani Kagera, ambako kuna kampeni kubwa ya kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.
“Tumekubaliana, serikali itatoa fedha kujengwe hospitali maalum kama ilivyo Mloganzila na hiyo ni kutokana na nature ya Kagera, imekua ikipatwa na majanga mengi,” amesema Ummy na kuongeza:
“Matishio mengi yanatokea Kagera, kama sio Kagera basi ni Kigoma au Katavi, serikali tumeliona hilo, tukakubaliana kuna haja ya kujenga hospitali maalum kama ilivyo Mloganzila, ” amesisiza.
Amesema hospitali hiyo itakua na miundombinu mizuri ya kuweka wahisiwa inapotokea mlipuko wa ugonjwa na watu wanaofuatiliwa, ambao walikua karibu na mgonjwa.
Amesema ujenzi wa hospitali mpya utakua na faida nyingi, kama kutoa huduma yenye viwango na ubora wa juu, huduma za kibobezi bila kuwepo kwa changamoto za kimfumo na pia itapunguza rufaa za wagonjwa kwenda Bugando mkoani Mwanza.
“Mimi sioni shida kutumia gharama kubwa kudhibiti ugonjwa wa Ebola usiingie nchini, lakini usipoingia tunamshukuru Mungu, “amesema.