Hospitali Korogwe yapigwa jeki

MKUU wa Wilaya ya Korogwe, Jokate Mwegelo amelishukuru Shirika la Lions Club International kuungana na serikali katika kuboresha huduma ya afya.

Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dar es Salaam, wakati akikabidhiwa viti sita vya magurudumu ‘wheelchairs’, jenereta ya 10KVA pamoja na mashine sita za kidijitali kupimia mapigo ya moyo ‘Stethoscope’, kwa ajili ya kutumika Hospitali ya Wilaya Korogwe.

“Lions Club International mmefanya jambo la kupongezwa sana, na hii inamaanisha ninyi ni sehemu ya serikali kwa kuwa mmeshiriki katika juhudi za serikali kuboresha sekta ya afya,” amesema.

Mwakilishi wa Lions Club International, Bhavika Sajan amesema ni  kawaida ya shirika hilo kurejesha katika jamii, na wamekuwa wakihudumu nchini tangu mwaka 1960.

“Dira na malengo yetu ni kurudisha kwa jamii inayotuzunguka, huduma zetu zimejikita kwenye maeneo kama vile mazingira, kupambana na njaa, kisukari, macho pamoja na saaratani,” amesema Bhavika.

Habari Zifananazo

Back to top button