Hospitali saba kutoa huduma tiba asili

SERIKALI imebainisha hospitali za rufaa saba nchini ambazo zimeanza kutoa huduma shirikishi za tiba asili ambazo mgonjwa atachagua huduma ya dawa atakayopewa ikiwemo dawa za asili ama ya kisasa baada ya kupatiwa vipimo mbalimbali na daktari.

Imesema huduma hiyo imeshaanza miezi kadhaa na dawa aina 19 zimefikishwa katika hospitali hizo na waliopatiwa huduma hakuna madhara makubwa yaliyotokea ingawaje wanaendelea na utafiti.

Aidha, Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) imesema inaendelea kukamilisha utafiti wa dawa ya asili ya kushugulikia tatizo la tezidume kwa wanaume.

Hosptali hizo ni pamoja na Temeke, Morogoro, Dodoma General, Mwanza Sekou toure, Ausha Mount Meru, Tanga Bombo na Mbeya.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya,Profesa Pascal Ruggajo amesema hayo leo Dar es Salaam katika kongamano la pili la watalaam wa tiba asili ikiwa ni siku moja kabla ya maadhimisho ya siku ya tiba ya asili kwa Mwafrika.

Amesema kupitia huduma hizo shirikishi mgonjwa atachagua huduma ya dawa atakayopewa baada ya kupita kwa daktari na kufanyiwa vipimo vyote alivyohitajika.

Ametaja dawa za magonjwa yanayoweza kupatiwa dawa za tiba asili katika hospitali hizi kuwa ni pamoja na vidonda vya tumboni,pumu,ngozi,upumuaji,njia ya mkojo,magonjwa ya tumbo, kuungua moto na hata maumivu wakati wa hedhi.

“Tumeanza na magonjwa hayo lakini tunaendelea kufanya tafiti, hivyo tunawaomba wananchi waunge mkono huduma hizo,” amesema Profesa Ruggajo na kuongeza kuwa wataendelea kutambua dawa za asili.

Amesema serikali inaendelea kufanya uwekezaji mkubwa wa afya, chini ya wizara ya afya na inapongeza jitihada zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea kuboresha sekta hiyo.

Amesema kupitia kongamano hilo, wadau wa tiba asili, wakiwemo washiriki zaidi ya 200 watakuwa na maazimio ya namna ya kuboresha eneo la tiba asili, kutoa elimu lakini pia kuongeza utafiti ili kuhakikisha watanzania wanatumia dawa salama na zilizothibitishwa.

Amesema wataendelea kuhakikisha kuwa tiba asili zinaendelezwa na tayari wapo madaktari, wauguzi pamoja na wafamasia ambao wamepatiwa mafunzo kuhusiana na huduma hizo shirikishi.

Kuhusu dawa za asili kuwa na madhara amesema, hakuna dawa isiyokuwa na madhara hata zile zisizokuwa za asili nazo zina madhara, kubwa ni mgonjwa kufuata masharti kutoka kwa wahusika.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Tiba asilia Wizara ya Afya Dk Vumilia Liggie amesema, dawa za asilia katika Hospitali za umma zitaendelea kuongezeka kulingana na tafiti zinazofanyika.

“Kwenye hizi hospitali ukimaliza mchakato wote wa kuonana na daktari, ukifika kwenye hatua za dawa, mgonjwa ana uamuzi wa kuchagua dawa aitakayo,” amesema Dk Liggie na kuongeza kuwa zipo nchi za nje kama China na India ambao wanaelndelea kutumia dawa hizo.

Kuhusu dawa ya tezi dume, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR Profesa Said Aboud amesema wanaendelea kufanya utafiti wa dawa ya tezidume.

Kongamano hilo la pili la dawa asilia limewakutanisha wataalamu mbalimbali wakiwemo watunga sera,watumiaji wa dawa, watengenezaji na wanasayansi.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button