Hospitali ya Rufaa ya Bombo iliyopo mkoani Tanga, inakabiliwa na uhitaji wa damu salama zaidi ya chupa 600 kwa mwezi, huku uwezo uliopo ni kukusanya chupa 250 hadi 300 pekee.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Idara ya Maabara ya Damu katika hospitali hiyo , Sinde Ntobu wakati wa uchangiaji wa damu kwa hiari uliofanywa na Taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania, tawi la Tanga.
Amesema kuwa uhitaji wa damu kwa wagonjwa ni mkubwa katika hospitali hiyo, hivyo ameiomba jamii kuona umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari,ili kuokoa maisha ya wagonjwa wengi wenye uhitaji na huduma hiyo.
“Tunaomba jamii ijitole damu kwa hiari, kwani kwa sasa muitikio ni mdogo kwa wananchi kuchangia kwa hiari, hivyo amezitaka taasisi nyingine kuiga mfano wa Taasisi ya Bilal waliouonesha,”amesema Ntobu.
Mkuu wa shule ya wasichana katika taasisi hiyo, Sheikh Sajad Hassan amesema kuwa uchangiaji wa damu katika hospitali huwa wanajitolea kila mwaka, ikiwa ni ishara ya kuonesha moyo wa kujitolea kwa wahitaji mbalimbali hususani watoto na mama wajawazito waliopo hospitali wanaohitaji kuongezewa damu.
“Lengo la kuja kuchangia damu hapa tunaifungamanisha sadaka yetu na tukio la kuuawa kwa mjukuu wa Mtume Muhammad (S.A .W) Hussein Bin Allyy aliyeuwawa mwaka 61 Hijiria, huko Irak aliyekuwa akiipigania dini kwa lengo la kukemea mabaya na kuamrisha mema, aliyetoka kutetea wanyonge na wale waliodhulumiwa,” amesema.
Back to top button