Hospitali ya Rufaa Chato, mapinduzi mengine huduma za kibingwa nchini

HOSPITALI ya Rufaa ya Kanda Chato ilianza kujengwa mwaka 2017 na hadi kufika Julai 30, 2021 awamu ya kwanza ya mradi ilikamilika na kuanza kutoa huduma ambapo Julai 30, mwaka huu (2022) imeadhimisha mwaka mmoja wa kutoa huduma za afya.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Oswald Yapa, akizungumza katika mwaka mmoja wa maadhimisho hayo, anasema huduma zinazotolewa zaidi kwa sasa ni kwa wagonjwa wa nje.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela (katikati) akiwa ameambatana na Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Kanda ya Rufaa Chato, Dk Brian Mawala (kushoto) katika ukaguzi wa maendeleo ya hospitali hiyo.

Anasema pia kuna kliniki mbalimbali za madaktari bingwa ambazo zimeendelea kutoa huduma kwa wananchi sambamba na huduma za utoaji dawa na vifaa tiba na huduma za maabara ya kisasa zaidi.

“Sasa hivi hawaendi Bugando, (Mwanza) kutokana na vifaa vya kisasa kabisa tulivyonavyo katika hospitali yetu hii wananchi wa wilaya yetu ya Chato na mikoa ya jirani huduma hizo zinapatikana katika hospitali hii.

“Hii imesaidia kupunguza gharama za kwenda umbali mrefu na vilevile kupunguza muda ambao walikuwa wanasafiri na sasa wanautumia wakiwa katika eneo la huduma kwani tunazo huduma za radiology, tuna X-Rays na tunavyo vipimo vya moyo,” anasema Dk Yapa.

Anaongeza: “Tangu Hospitali ya Rufaa Chato imeanza kutoa huduma, imefanikiwa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 10,500 huku asilimia 90 ya wagonjwa wanaofika ni wale wenye bima ya afya, asilimia tisa wanatibiwa kwa pesa mkononi na asilimia moja hawana uwezo wa kulipia gharama za matibabu.”

Anasema wale ambao wanakuwa hawana uwezo hospitali hiyo hutibiwa kwa utaratibu maalumu wa msamaha ambapo asilimia moja ya wagonjwa hao wanaohitaji msamaha wamehudumiwa.

Dk Yapa anasema kwa sasa hospitali hiyo inapokea na kuwahudumia wagonjwa kutoka mikoa ya Geita, Kagera, Kigoma na baadhi ya wilaya za Shinyanga ikiwemo wagonjwa wa rufaa binafsi kutoka maeneo hayo.

“Hospitali ina vitanda 83, ambavyo ni vichache kutokana na kwamba bado kuna matumizi makubwa ya jengo la nje, lakini serikali inaendelea kukamilisha jengo la wodi lenye vitanda 201 ili kuongeza idadi ya wagonjwa wanaoweza kuhudumiwa.”

Anasema malengo ya hospitali ni kuhudumia kati ya wagonjwa 700 hadi 1,000 kwa siku na vitanda vya wagonjwa kufikia 800 kwani eneo lililotengwa kwa ajili ya mradi ni hekari 248 huku zikiwa zimetumika hekari 18 pekee na kusalia na eneo la hekari 230.

“Hospitali hii ilianza kujengwa kwa awamu ya kwanza ikiwa na jumla ya majengo manne, ambayo ni jengo la OPD ambalo limekamilika lenye ukubwa wa mita za mraba 2,900 na jengo la famasia na maabara lenye ukubwa wa mita za mraba 1,810.

“Hadi sasa kuna ujenzi unaendelea wa jengo la wagonjwa wa dharura lenye ukubwa wa mita za mraba 725 lakini vilevile kuna jengo la huduma ya uangalizi maalumu (ICU) lenye ukubwa wa mita za mraba 784,” anasema Dk Yapa.

Anasema kwa sasa hospitali hiyo ina jumla ya watumishi 227 pekee ikiwemo watumishi 84 kutoka ajira mpya za mwaka 2022 na ujenzi utakapokamilika kwa asilimia 100 uhitaji utafikia watumishi 1,164.

Anaeleza uwepo wa Hospitali ya Kanda Chato imesogeza upatikanaji wa huduma za dharura, wagonjwa mahututi, magonjwa ya matibabu ya kibingwa ikiwemo moyo, kisukari, magonjwa ya watoto, wanawake na upasuaji.

Maboresho ya huduma na miundombinu

Akizungumza katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela alipotembelea hospitali hiyo mapema Agosti 2022, Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Kanda ya Rufaa Chato, Dk Brian Mawala anasema wameanza kutoa huduma za kibingwa katika fani ya upasuaji.

Dk Mawala anasema pia wanatoa huduma ya mama na mtoto na bado wanakamilisha kufungua kitengo cha kusafisha damu na jengo la Wagonjwa Mahututi (ICU).

“Katika Mradi wa Kukabiliana na Madhila ya Virusi vya Corona (TCRP) hospitali imepokea takribani Sh bilioni 6.2 ambapo kwenye jengo la mionzi (radiolojia) mashine za MRI na CT-Scan zinaenda kununuliwa ambazo ni mashine muhimu kwa huduma ya kanda,” alisema Dk Mawala.

Meneja wa Wakala wa Majengo (TBA) Mkoa wa Geita, Gladys Jefta ambao ni wakandarasi wa mradi, anasema awamu ya kwanza ya ujenzi imegharimu Sh bilioni 13 na imekamilika kwa asilimia 99 na tayari awamu ya pili imeshaanza.

“Lakini pia kuna awamu ya pili na tunaendelea na ujenzi ambapo kuna jengo la huduma ya mionzi ambalo limeshakamilika na linatoa huduma, lakini pia tuna jengo la wodi ambalo litakuwa na vitanda 201 ambalo tunaendelea na utekelezaji upo asilimia 76.

“Pia kuna kazi za nje kama njia za kupitishia wagonjwa, maegesho ya magari, mifumo ya maji safi na maji taka. Awamu ya pili ya mradi huu ina gharama ya Sh bilioni 18 na mpaka sasa TBA tumeshalipwa Sh bilioni tisa na ujenzi unatarajiwa kukamilika Novemba 2022,” anasema Jefta.

Juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika mradi

Mkuu wa Wilaya ya Chato, Martha Mkumpasi anakiri tangu kuanza kwa mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato mpaka sasa serikali imeidhinisha takribani Sh bilioni 35 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na maboresho ya miundombinu na kwa usimamizi makini, imara, thabiti na shirikishi kazi inaendelea.

“Sisi kama serikali tuna majukumu kama matatu, kwanza ni kuhakikisha majengo yote yanakamilika kwa wakati, lakini pili kuhakikisha kwamba yanajengwa kwa viwango na tatu kuhakikisha kwamba hakuna ufujaji wa fedha,” anasema Martha.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Shigela anabainisha ili kuboresha huduma, serikali tayari imeshatoa Sh bilioni 7.2 katika bajeti ya mwaka fedha 2022/2023 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato.

Anasema kati ya fedha hizo, tayari Sh bilioni saba kimeshapelekwa Bohari ya Dawa (MSD) ambao walipeleka hospitalini hapo vifaa tiba vya thamani ya Sh bilioni 2.4 na Septemba 2022 wanatarajiwa kupeleka mashine za MRI na CT Scan zinazogharimu jumla ya Sh bilioni 4.5.

“Kwa hiyo Serikali ya Awamu ya Sita inafanya kazi kubwa, tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha kwamba misingi mizuri ambayo walianza pamoja na Dk John Magufuli katika awamu ya tano, anaiendeleza katika awamu ya sita kwa kasi kubwa zaidi.

“Nina uhakika kwamba ukamilishaji wa huduma hizi, tutakuwa na huduma bora zaidi kwa wananchi wetu wanaozunguka katika mkoa wetu huu wa Geita, tutaokoa maisha ya Watanzania waliokuwa wanapelekwa mpaka Mwanza au Dar es Salaam,” anasema Shigela.

Shigela anawahakikishia wananchi wa Chato mkoani Geita na maeneo ya jirani kuwa atamsaidia Rais Samia kusimamia kikamilifu kukamilika kwa hospitali hiyo ili kufikiwa malengo ya kuboresha huduma za afya nchini hususani zile za kibingwa.

Mtazamo wa wananchi juu ya mradi

Mkazi wa mjini Geita, Hussein Rubara akizungumza baada ya kupata huduma hospitalini hapo anaipongeza serikali kwa kuendelea kukamilisha hospitali hiyo kwani inasogeza vipimo vya kibingwa karibu na wananchi.

“Tunafarijika kwa sababu hospitali imetangaza ina vipimo vikubwa na salama vya magonjwa sugu, mimi binafsi nimefuata vipimo vya shinikizo la damu, magonjwa ya moyo na figo. Nimefika hapa nimeona huduma ni nzuri kwani nimepokelewa vizuri na kupata majibu kwa wakati,” anasema Rubara.

Naye Alveria Nicolous anakiri kujengwa kwa hospitali hiyo kumewapa uhakika wa kupata huduma za kibingwa na kufufua matumaini kwa wananchi ambao awali walihofia kutumia muda mrefu na gharama kubwa kufuata huduma za kibingwa nje ya Mkoa wa Geita hasa zaidi Bugando.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button