MBUNGE wa Jimbo la Ulanga mkoani Morogoro, Salim Alaudin Hasham ametoa msaada wa gari jipya la kisasa aina ya Toyota Land Cruiser la kubeba wagonjwa lenye thamani ya Sh milioni 120 kwa Hospitali ya Wilaya ili kurahisisha utoaji huduma za matibabu kwa wananchi.
Mbunge huyo amekabidhi gari hilo wakati Tamasha la kumpongeza Rais, Dk Samia Suluhu Hassan na mbunge huyo lililofanyika mjini Mahenge ambalo liliandaliwa na Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Ulanga ikiwa ni kutambua mchango wa Rais na Mbunge kwa namna walivyowawezesha vijana kiuchumi na kujiajiri.
Amesema lengo kubwa la kununua gari hilo ni kuunga mkono juhudi za Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya afya kwa sababu bado kuna changamoto nyingi licha ya yeye ( Rais) amefanya na anaendelea kufanya mambo makubwa .
“ Nimetoa fedha mfukoni kwangu kununua gari hili lengo ni kuunga mkono juhudi za mheshimiwa Rais wetu na lengo kubwa zaidi ni kuwasaidia wananchi wa jimbo langu ambao waliniamini kwa kunichangua kwa kura nyingi , na mimeamua kufanya haya kutoka kwenye moyo wa sakafu yangu” amesema Salim
Mbunge huyo amesema ,katika hospitali hiyo ipo huduma za gari lakini ni ya zamani aina ya Toyota Hiace, ambayo imetumika kwa muda mrefu na imechoka, hivyo gari jipya la kisasa lililonunuliwa ni imara zaidi na litaweza kukidhi mahitaji ambayo wananchi wanayahitaji
“ Nimetumia fursa katika tamasha hili kukabidhi gari la wagonjwa lenye thamani ya Sh milioni 120 kwa wananchi wa Ulanga, lengo la gari hili ni kwa ajili ya wagonjwa wanaopata rufaa kutoka vijijini kufikishwa Hospitali ya wilaya au kutoka nje ya Hospitali ya wilaya na wanauwezo wa kulitumia gari hili” amesema Salim
Mbunge huyo amesema kuwa , jukumu la wananchi ni kuweka mafuta pekee na kwamba gharama nyingine zote zitakuwa chini ya Ofisi ya Mbunge wa Jimbo hilo.
Mbali na hilo alitaja fursa nyingine kwa matumizi ya gari hilo ni kwa Mwananchi yoyote ambaye atakuwa amefiwa awe anaishi ndani ya Jimbo hilo au nje ya jimbo , jukumu lake endapo anahitaji kurudisha mwili wa ndugu yake , anatajibika kuweka mafuta na gari litafanya kazi ya kwenda kuhudumia.
“Huduma hii ni kwa Mwananchi ambaye amefiwa awe ndani ya Jimbo la Ulanga au nje ya jimbo hilo , iwe Mwanza , Tabora , Kigoma na mikoa mingine yeye jukumu lake napohitaji kurudisha mwili wa ndugu yake nyumbani kwa maana ya jimboni ni kuweka mafuta ya gari “ amesema Salim
Kwa upande wake Kaimu Mganga mkuu wa wilaya ya Ulanga , Dk Stephano Liwemba licha ya kumshukuru Mbunge huyo kwa kuwapatia gari jipya ,amesema serikali haikombali kwani imeendelea kuimalisha huduma za afya kuanzia ngazi ya Zahanati, Vituo Vya Afya na kwenye ngazi za Hospitali.
Dk Liwemba amesema Hospitali hiyo ni kongwe ambayo imejengwa mwaka 1905 na wakoloni wa Kijerumani na imeendelea kukarabatiwa na kufanyiwa upanuzi kwa baadhi ya majengo , lakini haina mpangilio mzuri kwa sasa na haina uzio na ipo kati kati ya mji.
Amesema kwa sasa Hospitali hiyo inahitaji kuwa na maabara ya kisasa ili kukidhi mahitaji ya ongezeko la wananchi kwani iliyopo ni ndogo n a ni ya kizamani.
Dk Liwemba amesema Hospitali hiyo inahitaji kuwa na jengo la kisasa la upasuaji na vifaa vya kisasa kwa vile linatumika lilijengwa na wakoloni na kwa sasa halikidhi mahitaji makubwa kwa hadhi ya hospitali ya wilaya .
“ Kwa sasa wilaya inaongezeko kubwa la wananchi kutokana na shughuli za akiuchumi zinazofanyika , wilaya imekuwa na mwingiliano wa watu ni mkubwa , hivyo inahitajika kujengwa hospitali kubwa ya wilaya itakayokuwa na vifaa vya kisasa kukidhi mahitaji ya wananchi” amesema Dk Liwemba.