Hospitali zatakiwa kuwapima Selimundu watoto wanaozaliwa
DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu amezitaka hospitali zote za halmashauri nchini kuwapima Ugonjwa wa Selimundu watoto wote wanaozaliwa katika hospitali hizo ili kujua hali zao mapema na kuanza matibabu.
Kiongozi huyo, ameeleza hayo leo wakati akizindua kampeni ya kuelimisha jamii juu ya magonjwa yasiyoambukiza, jijini Dar es Salaam.
“Waganga Wakuu wa Mikoa mkalisimamie hili, nataka Hospitali zote za Halmashauri nchini ndani ya miezi sita zipime ugonjwa wa Selimundu kwa watoto wanaozaliwa katika Hospitali hizo kabla sijashuka vituo vya Afya,” amesema Waziri Ummy
Waziri Ummy amebainisha kuwa zaidi ya asilimia 70 hadi 90 ya watoto wanaozaliwa na Selimundu hupoteza maisha ndani ya kipindi cha miaka mitano ya mwanzo wa maisha yao kutokana na kutotambulika au kwa sababu ya unyanyapaa na kukosa elimu.
“Hali hii haikubaliki ni lazima tuchukue hatua za haraka ili kuokoa maisha ya watoto wachanga wenye ugonjwa wa Selimundu kwa kuwatambua mapema ili kuhakikisha wanapata matibabu kwa wakati,” amesema Kiongozi huyo.
Aidha, ametanabahisha kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anatoa fedha za dawa kwa asilimia 100 kila mwezi, fedha hizo wanaruhusiwa kuzitumia kwa ajili ya kununua mashine za kupima ugonjwa wa Selimundu.