Hotuba ya Rais Samia inatosha kumvua chui ngozi ya kondoo

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Samia Suluhu Hassan, ameendelea kusimamia ukweli na kuipa kisogo batil kuitupa katika kaburi la sahau.

Mwenyekiti wa Chama na Rais Dk Samia, katika  hotuba  yake ya kufunga Mkutano Mkuu wa 10 wa CCM uliomalizika jioni ya Desemba 8, Dodoma imewakosha wengi, sio tu wanachama wa CCM bali umma wa watanzania kwa ujumla.

Mwenyekiti wa CCM ametamka kweupe kwamba wapo watendaji katika serikali hawaendani na kasi yake na hivyo ataisuka upya serikali ikiwa ni dhamira ya kuongeza kasi ya utendaji serikalini.

Matamshi  ya Mwenyekiti Dk Samia yameakisi mtazamo wa wengi, kwa hakika mawaziri na watendaji wetu wengi wao wamejawa na maneno mengi kuliko vitendo.

Hotuba ya jana imewakosha wananchi na kuwapa matumaini mapya ya mambo mazuri zaidi yanakuja, ambapo mabadiliko ya serikali yatatosha kuwavua chui waliojivika ngozi ya mwanakondoo.

Mwenyekiti, Rais Dk  Samia amevunja ukimya juu ya baadhi ya watu wanaodhani kuwa upole wake ni udhaifu na wakidhani hivyo itakuwa kioo kimewacheza. Hotuba ile  ya Mwenyekiti ni hotuba ya Kimapinduzi.

Nasema ya kimapinduzi ni kwa sababu italeta chachu ya mageuzi sio tu ndani ya CCM bali katika serikali.

Wananchi wanahitaji shida zao kutatuliwa, wanahitaji kupata mkate wao, wanahitaji huduma za kijamii na wanaotakiwa kuyafanya haya kwa niaba ya serikali ni watendaji.

Mabadiliko yataleta ufanisi katika utendaji wa serikali na kuondokana na ile fikra ya kudhani kuwa serikalini ni sehemu ya kuvuna mali.

Kwa hakika, hotuba yake  Mwenyekiti katika Mkutano Mkuu wa CCM  imewafungua macho Watanzania, sasa wanafahamu mbichi na mbivu, sasa wanafahamu ukweli wa mambo.

Nimemsikiliza kwa makini sana Mwenyekiti Rais Dk Samia na katika uelewa wangu ni kuwa hotuba yake ni dira na muelekeo wa serikali anayoiongoza inavyotakiwa iwe.

Ingekuwa vizuri zaidi hotuba yake ikawekwa katika  mfumo wa vitini, ikawa mada mojawapo ya kuwafunza viongozi wapya ndani ya CCM.

Kwa wale ambao walijificha katika kivuli cha uzalendo huku matendo yao si ya wema, jinsi usiku unavyoingia na giza kutanda, ndivyo mapambazuko ya ukweli dhidi ya ufisadi na wale wenye mwendo wa kinyonga unavyokaribia mwisho wao.

Waswahili wanasema ” Usiku wa deni haukawii kucha” . Wapo waliodhani kuwa ndio wamefika, hakuna mabadiliko wao ndio ” ALFA NA OMEGA” sasa leo matumbo joto.

Ni ukweli usiopingika kuwa uongozi wa Rais Dk Samia ni uongozi wenye kuwajali wananchi.

Ujio wake akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk  Samia ameturejeshea furaha yetu, ametufanya kuwa wamoja zaidi, lakini kukirudisha chama cha CCM katika desturi yake, mazoea yake, ambapo wajumbe wanapata fursa ya kuchangia na kujadili mambo ya chama chao.

Mwenyekiti Dk Samia hakufanya Mkutano Mkuu wa CCM kwa saa kadhaa, bali amefanya Mkutano Mkuu wa 10 kwa siku 2 huku kila anaetaka kusema anasema.

Hakuna kusemea kwenye vibuyu, kila mtu aseme peupeni tena bila kuwa na hofu.

Mwenyekiti na Rais Dk  Samia hana chuki na mtu, hana ubaya na mtu na wala hana roho mbaya, wananchi wote kwake sawa.

Tuna kila sababu ya kuipongeza hotuba ya Mwenyekiti Rais Dk Samia na isiishie katika pongezi tu bali ifanyiwe kazi yale yote ambayo ameyaelekeza kwa watendaji wa CCM, viongozi na watendaji wa serikali kwa upande mwengine.

 

Habari Zifananazo

Back to top button