Huduma za usuluhishi zitiliwe mkazo kortini

FEBRUARI 2 ya kila mwaka Mahakama ya Tanzania huadhimisha Siku ya Sheria, ikiwa na lengo la
kuashiria mwaka mpya wa mahakama.

Katika siku hiyo, mahakama hutathmini mafanikio na changamoto kwa mwaka uliopita na kupanga mikakati ya kuboresha utendaji wa mahakama kwa mwaka huu.

Mwaka huu wiki ya sheria imekuwa ikielimisha wananchi kuhusu usuluhishi wa mashauri mbalimbali
nje ya mfumo rasmi wa mahakama.

Advertisement

Usuluhishi unatajwa kuwa njia bora na ya haraka kwa wadaawa kwani hupunguza muda na gharama ya uendeshaji wa kesi hivyo wananchi wafuate utaratibu huu ili kesi ambazo hazina ubishani wa kisheria kuisha kwa kufuata utaratibu wa usuluhishi katika vituo na mabaraza.

Hata hivyo, miongoni mwa mambo ambayomahakama imefanikiwa na inapaswa kuigwa na taasisi nyingine ambazo zinahusika na utoaji haki, ni matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano katika uendeshaji wa shughuli zake ikiwemo uendeshaji wa mashauri ya jinai na madai.

Pia mahakama hiyo imefanikiwa kuhakikisha inaendeleza maboresho kwa majengo ya mahakama za mwanzo, wilaya na mikoa kwa ajili ya kuhakikisha ufanisi katika utoaji haki.

Mambo mengine ambayo mhimili huo unajivunia ni uharakishaji wa mashauri, kudhibiti upotevu wa majalada ambapo sasa inasajili majalada yote ya kesi kidijitali kwa mfumo rasmi wa mahakama ambapo kila mdau anayehitaji huduma za mahakama huzipata pasi kufika mahakamani.

Sambamba na hilo mahakama imeweza kuhakikisha inatoa mafunzo mbalimbali kwa watumishi wake kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wake, kukemea ukosefu wa maadili ikiwemo upokeaji wa rushwa ili kuifanya mahakama hiyo kuaminiwa na wananchi.

Katika masuala ambayo yalikuwa yakiikabili mahakama na Rais Samia Suluhu Hassan ameyakiri wazi ni kukithiri kwa vitendo vya upokeaji rushwa kwa maofisa wa mahakama. Kwa muda mrefu mhimili huo umechangia wananchi kukosa imani na mahakama kutokana na vitendo hivyo vinavyominya haki za watu
wengine.

Pamoja na jitihada mbalimbali za kudhibiti rushwa mahakamani, lakini bado vitendo hivyo vinaripotiwa hivyo kuifanya mahakama kuwa miongoni mwa taasisi zitakazochunguzwa na tume ya haki jinai
iliyozinduliwa jana.

Sababu nyingine zinazoifanya mahakama katika uchunguzi ni ucheleweshaji wa kesi ambao wakati mwingine huchangiwa na waendesha mashitaka na polisi ambao ni wapelelezi hivyo tume hiyo itabainisha mapendekezo
yao ya namna ya kurahisisha utoaji haki.

Hata hivyo, mahakama pekee haiwezi kukamilisha masuala ya utoaji haki bila wadau wengine ambao nimawakili wa kujitegemea, mawakili wa serikali, polisi, Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Rais Samia alisema kuwa suala la uchepushaji wa haki ni miongoni mwa vitu vibaya duniani kwa sababu watu wanaingia hatiani kwa kusingiziwa kesi na wengine kukosa haki zao. Lakini pia katika kupunguza mahabusu magerezani, mahakama iendelee kuhakikisha inatoa masharti nafuu ya dhamana ili watuhumiwa
waweze kudhaminiwa, hivyo itasaidia kuondoa mrundikano wa mahabusu.

Ni vema kutambua kuwa suala la utoaji haki kwa wakati ni miongoni mwa mipango ya maendeleo endelevu kwa nchi kwa sababu, huvutia wawekezaji toka mataifa mbalimbali na kukuza ustawi wa jamii. Hivyo ni lazima kila
mdau wa mahakama ahakikishe anaisaidia mahakama kutoa haki kwa wakati ili kurudisha imani ya wananchi.