IAA watangaza udhamini wa masomo kozi 5 mpya

KATIKA kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan, Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kimetangaza udhamini wa masomo katika kozi mpya tano za kimkakati kwa mwaka 2023/2024

Akitangaza udhamini huo leo Agosti 24, 2023 jijini Dar es Salaam, Mkuu wa chuo hicho Profesa Eliamani Sedoyeka amesema kozi hizo ni shahada ya ukaguzi wa hesabu na uhakikisho, shahada ya media anuwai na mawasiliano kwa umma, shahada ya usimamizi wa nyaraka na taarifa, shahada ya usimamizi wa mikopo na shahada ya ukutubi na sayansi ya taarifa.

Profesa Sedoyeka amesema udhamini huo unawalenga wahitimu wa kidato cha sita kwa mwaka 2022 na 2023 wenye ndoto na malengo ya kusomea fani tajwa na wale wanaokabiliwa na changamoto za kifedha.

Aidha, ametaja vigezo vya kupata udhamini huo kuwa ni muombaji awe na ufaulu mzuri katika mtihani wa kidato cha nne na sita, usawa wa kijinsia, uthibitisho wa uhitaji wa msaada wa udhamini wa masomo.

“Vigezo hivyo pekee havitoshi ni lazima muombaji atoe maelezo ni kwa nini anadhani anastahili kupata mkopo, kusema hana uwezo haitoshi, atoe sababu za kutushawishi zaidi.

” amesema Sedoyeka na kufafanua:

” Mfano kuna mwandishi mzuri wa michezo lakini ana Diploma hivyo angependa kusoma shahada ya Media Anuwai na Mawasiliano kwa Umma, anatueleza uzoefu wake katika uchambuzi wa michezo hivyo anaona akipata udhamini huo akaongeza elimu atakuwa bora, vigezo kama hivyo, ” amesema.

Profesa Sedoyeka amesema pia, ili muombaji akidhi vigezo vya kupata udhamini ni lazima awe ameomba kujiunga na chuo cha IAA na kufanya udahili.

“Dirisha la udahili awamu ya pili limefunguliwa rasmi leo Agosti 24 hadi Septemba 3, 2023.” amesema Prof. Sedoyeka

Prof. Sedoyeka ametoa wito kwa wanafunzi wote wenye Nia na hamasa ya kusoma katika chuo hicho cha IAA kuchangamkia fursa hiyo na kuomba udhamini.

…….

Habari Zifananazo

3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button