Idadi watu wenye ulemavu yaongezeka

DODOMA; KIWANGO cha watu wenye ulemavu nchini kimeongezeka hadi asilimia 11.2 mwaka 2022 kutoka asilimia 9.3 ilivyokuwa mwaka 2012, Bunge limeelezwa.

Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande ametoa maelezo hayo bungeni leo Juni 4, 2024, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Stela Ikupa, aliyehoji kama Serikali imekamilisha kuchakata na kufahamu idadi ya watu wenye ulemavu kwa kila halmashauri kwa mujibu wa sensa 2022.

“Kwa sasa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekamilisha uchakataji wa taarifa za sensa za hali ya ulemavu katika ngazi zote za utawala.

“Kwa ufupi matokeo yanaonesha kuwa, kiwango cha watu wenye ulemavu wa aina yoyote ile nchini kimeongezeka hadi asilimia 11.2 mwaka 2022 kutoka asilimia 9.3 ilivyokuwa mwaka 2012,” amesema Naibu Waziri.

“Aidha, kuna kiwango kikubwa zaidi cha wanawake wenye ulemavu (asilimia 11.6) ikilinganishwa na wanaume (asilimia 10.9).

“Mheshimiwa Spika, Matokeo  ya Sensa ya mwaka 2022 yamechambuliwa hadi ngazi zote za utawala  na kwa sasa Ofisi ya Taifa ya Takwimu na ile ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar  wanakamilisha kutengeneza kanzidata ya watu wenye ulemavu hadi ngazi ya kitongoji ambayo imelenga kuwatambua walemavu wote kwa majina, mahali wanapoishi, na namba za simu za mikononi kama zilivyokusanywa Agosti 2022 na taarifa nyingine za kijamii, kiuchumi na mazingira ya kundi hili.

“ Kanzidata itazinduliwa ndani ya mwaka wa fedha 2023/24,” amesema Naibu Waziri huyo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button