Idadi ya Mawakili wa kujitegemea yavuka 11,000

JAJI Mkuu wa Tanzania Prof Ibrahim Hamis Juma amewataka Mawakili wapya 358 kufungua ofisi karibu na Mahakama za Wilaya nchi nzima ili kurahisisha upatikanaji wa msaada wa sheria kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuwakubari na kuwapokea mawakili hao katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sherehe za 67 za kuwakubali na kuwaingiza kwenye daftari la Mawakili, Prof Juma amesema sasa kuna Mawakili 11,084 wa kujitegemea nchini Tanzania.

Tangu mwaka 2015 Mahakama ya Tanzania imejenga majengo ya kisasa ili kutoa huduma za Mahakama katika mikoa yote ya Tanzania. Majengo 20 ya Mahakama za Wilaya ambayo yamezinduliwa hivi karibuni yamelenga kuwezesha Mahakama ya Tanzania kusogeza huduma ya utoaji haki karibu na wananchi.

Advertisement

Wilaya hizo ni pamoja na Mwanga , Same, Busega, Itilima, Butiama Rorya , Songwe , Gairo ,Mkinga , Mbogwe, Nyang’hwale, Kyera, Missenyi, Kaliua, Uvinza , Buhigwe, Kakonko, Tanganyika,Kilombero na Mvomero.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, uwepo wa mahakama hizo ni fursa kwa mawakili wapya.

Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) Prof. Edward Hoseah aliwataka Mawakili wapya kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili yaliyopo katika viapo vyao ili waweze kuepuka kujiingiza katika matatizo ya ukiukaji wa maadili ambayo yanaweza kuwasbabishia kukosa sifa ya kuendelea na utoaji wa huduma hiyo.

Alisema watakaobainiki kukiuka maadili watachukuliwa hatua kwa mujibu na taratibu na Sheria zinazolinda viapo vyao kama Maafisa wa Mahakama na kuna uwezekano wa kuondolewa katika daftari la Mawakili.

Prof. Hoseah aliongeza kuwa Chama cha Mawakili Tanganyika kinaendelea kupambana na vishoka ambao wamekuwa wakiendesha vitendo haramu na visivyo vya kimaadili ya kiutendaji kazi za uwakili na kuchafua taaluma hiyo muhimu kwa maendeleo ya Nchi.

Alisema vitendo hivyo vimekuwa vikisababisha kushuka kwa hadhi ya taaluma ya Uwakili na kusababisha kutoamini na Serikali na wadau mbalimbali katika jamii.

“Kuna baadhi ya watu wanaofanyika kazi za uwakili ingawa wao sio mawakili.watu hawa wamekuwa wakifanya kazi mbalimbali za kiuwakili kama vile kuandaa nyaraka , kuthibisha nyaraka , kushuduhia viapo. Wahalifu wa vitendo viovu ni watu wanaojifanya ni mawakili lakini sio mawakili, tunaendelea kupambana nao”alisisitiza.

Kwa upande wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Eliezer Feleshi alisema kumekuwepo na tabia ya baadhi ya Mawakili kujisahaulisha au kutoutendea haki wajibu wao wa kuisaidia Mahakama kufikia maamuzi ya haki kwa wakati.

Alisisitiza kuwa hiyo siyo tu kwamba si jambo jema lisilo na maadili, bali, linawaondolea baadhi hadhi ya kuwa Mafisa wa Mahakama wanapotekeleza wajibu wake kwa wateja wao.

Ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi,Alisema Mawakili ambao watashindwa kujiendelea ipo hatari kwao kujikuta wakinukuu Sheria ambayo imeshafanyiwa mabadiliko na haitumi tena.

“Kwa mfano, wakili anapoamua kufanya rejea kwenye uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani, anapaswa kusoma uamuzi wote na kuuelewa na siyo kutumia aya moja ya uamuzi huo hivyo kuipotosha Mahakama pamoja na kwamba Mahakama nayo inalo jukumu la kuusoma ili kujiridhisha na usahihi wa hoja kwa mujibu wa uamuzi rejewa,” alisisitiza.

/* */