Idadi ya watalii yaongezeka kwa asilimia 96
DODOMA; WIZARA ya Maliasili na Utalii, imesema kumekuwa na ongezeko la idadi ya watalii wa kimataifa kwa asilimia 96.
Akiwasilisha makadirio na mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25 bungeni mjini Dodoma leo Mei 31, 2024, Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki, amesema idadi hiyo imeongezeka kutoka watalii 922,692 mwaka 2021 hadi watalii 1,808,205 mwaka 2023.
“Aidha, idadi ya watalii wa ndani waliotembelea vivutio vya utalii imeongezeka kwa asilimia 152 kutoka watalii 788,933 mwaka 2021 hadi kufikia watalii 1,985,707 Mwaka 2023.
“Kuongezeka kwa mapato yatokanayo na shughuli za utalii ambapo mapato yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.3 Mwaka 2021 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 3.4 Mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 161 kwa watalii wa kimataifa.
“Pia, mapato yatokanayo na utalii wa ndani yameongezeka kutoka Sh. bilioni 46.3 mwaka 2021 hadi Sh bilioni 175.3 waka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 279.
“Aidha, ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali uliongezeka kutoka Sh 397,428,671,968 mwaka 2020/2021 hadi Sh 680,150,218,337 mwaka 2022/2023.
“Vilevile, kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 kuanzia Julai 2023, hadi kufikia Aprili 2024, Wizara imekusanya jumla ya Sh 750,992,839,479.75 sawa na asilimia 97.12 ya lengo la makusanyo,” amesema Waziri Kairuki.