IFM Mwanza wachangia damu

IFM Mwanza wachangia damu

WATUMISHI na wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa fedha (IFM) Kampasi ya Mwanza, wamechangia damu, ikiwa ni sehemu ya kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya taasisi hiyo.

Mratibu Taaluma IFM, John Euseby, amesema maadhimisho hayo yaliyoanza mwaka jana yamekua yakihusisha shughuli na michango mbalimbali, ikiwemo kutoa msaada wa vifaatiba katika Zahanati ya Kirumba, wilayani Ilemela.

“Kadhalika tumetoa mafunzo ya kitaaluma kwa viongozi wa serikali za mitaa, wakiwemo madiwani katika Wilaya ya Ilemela na Misungwi, juu ya uibuaji miradi ya maendeleo na namna bora ya kuisimamia, kwa maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Advertisement

“Na leo hii tunachangia damu ili  kunusuru maisha ya wenzetu huko hospitalini,” amesema.

 

Ofisa Uhamasishaji wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Burton Zakaria, amepongeza juhudi za wanajamii wa IFM kuchangia damu, akawaomba wanajamii wote kuunga mkono jitihada kwani mahitaji bado ni makubwa.

Amesema uhitaji kwa Kanda ya Ziwa ni chupa 200 za damu kwa siku, kiasi ambacho hakijawahi kutimia licha ya kampeni za uhamasishaji sehemu za mikusanyiko mbalimbali ya watu, ikiwemo nyumba za ibada, mikutano ya hadhara na shuleni.