IFRC kuanzishwa nchini

SERIKALI ipo mbioni kuanzisha ofisi za Shirikisho la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (International Federation of Red Cross and Crescent – IFRC) hapa nchini.
Hayo yamesemwa  na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Patrobass Katambi na kwamba serikali ipo kwenye mchakato wa mwisho wa kukamilisha usajili wa shirika hilo la IFRC.

Katambi ameyasema hayo akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mufindi Kusini David Kihenzile,  lililoulizwa kwa niaba na Mbunge wa Viti Maalumu Judith Kapinga ambaye alihoji ni lini Serikali itakamilisha usajili wa Shirikisho la International Federation of Cross and Crescent nchini?
Akijibu swali hilo Katambi alimpongeza Kihenzile ambaye pia ni Rais wa Red Cross Tanzania,  kwa kusimamia mchakato huo kwa muda mrefu na kwamba sasa serikali inaenda kuuhitimisha.
“Kwanza niwapongeze Redcross Tanzania wamekuwa wakisimamia mchakato huu kwa kipindi kirefu sana, na wamehakikisha hatua hii imeanza kufikiwa, wamekuwa wakifanya kazi kubwa katika sheria mbali mbali za kitaifa na kimataifa, kusimamia maafa, wamekuwa wadau muhimu wa serikali katika masuala ya maafa.”Amesema Katambi na kuongeza
“IFRC ni shirika la kimataifa linalounganisha vyama vya nchi mbalimbali vya Msalaba Mwekundu. Nchini Tanzania, Chama cha Msalaba Mwekundu kilianzishwa chini ya Sheria Na. 71 ya mwaka 1962 kufuatia nchi yetu kuridhia Mikataba ya Geneva ya mwaka 1949.

” Amesema Katambi na kuongeza

Advertisement

“Kazi kubwa ya Shirikisho hili ni kufanya shughuli za kusaidia wahanga wa maafa na kuimarisha uwezo wa wanachama wake katika kukabiliana na maafa.
kutokana na umuhimu wa Shirikisho hilo kwa nchi yetu, Serikali iko katika hatua za mwisho kukamilisha mkataba na Shirikisho hilo.”Amesema
Amesema hatua hizo zitakapokamilika Mkataba utasainiwa na Ofisi za IFRC kufunguliwa nchini na kuanza kufanya kazi.
Aidha, akijibu swali la nyongeza liloulizwa na Judith Kapinga, ambae alitaka kufahamu ni  lini mchakato huo utakamilika rasmi kwa vile umechukua muda mrefu takribani miaka 30, na serikali imejipangaje kuhakikisha shirika hilo litakapoanza kazi ajira za watanzania zitakuwepo, Katambi amesema tayari itifaki zote zimeshafanyika ili kukamilisha mchakato huo.
“Kwanza kwa kuwasiliana na shirikisho lenyewe, lakini pili kukutana na wadau na tatu sasa hivi tupo kwenye hatua ya Wizara ya Mambo ya Nje kukamilisha hitifaki za kiserikali na taratibu za ndani ili kuhakikisha jambo hili linakamilika, ndio maana tukasema sasa limefikia mwisho.”Amesema
Kuhusu maslahi amesema mashirika ya kimataifa yamekuwa yakifanya kazi hapa nchini lakini serikali imekuwa ikiangalia  ajira za wazawa kwa mujibu wa sheria iliyopitishwa na bunge mwaka 2005 inayohusu uratibu wa ajira za wageni.
“Imekuwa ni wakati wote hata katika usajili wa makampuni sura namba 212 inaelekeza inaposajiliwa kampuni, taasisi au asasi za kiraia, sharti ni kwamba lazima waajiri watanzania, na inapotokea ameajiriwa mgeni ni pale tu ambapo taaluma yake ni maalum sana au maarifa aliyonayo hapa nchini  huwezi mpata Mtanzania mwenye sifa hizo.
“Nitoe rahi waajiri waitekeleze sheria hii,  usajili utakua chini ya redcross tutawaomba waratibu ili watanzania waweze kuajiriwa.”Amesema