TIMU ya soka ya Ikongosi (Ikongosi FC) imejinyakulia seti moja ya jezi na mpira wa kisasa baada ya kuibamiza kwa bao 1-0 Itulavanu FC katika fainali ya Negro Bonanza iliyopigwa katika uwanja wa kijiji cha Lugongo katika kata ya Ikongosi wilayani Mufindi.
Diwani wa kata ya Ikongosi, Negro Sanga aliyedhamini bonanza hilo lililohusisha pia mpira wa pete, mbio za kwenye magunia na kufukuza kuku ametumia bonanza hilo kutoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Washindi wa michezo hiyo walijinyakulia fedha taslimu ya kati ya Sh 20,000 na Sh 100,000 huku wakiomba bonanza hilo liwe linafanyika kila baada ya miezi miwili.
Akikabidhi zawadi kwa washindi Sanga amesema anatambua michezo ni afya lakini pia ni ajira kama itaendelezwa ipasavyo.
“Mpira wa miguu ni njia nzuri ya kukuza vipaji vya wachezaji. Kuendeleza michezo kwa vijana hutoa fursa ya kujifunza stadi za timu, ushirikiano, na uongozi. Pia, inaweza kusaidia katika kujenga afya bora na kutoa jukwaa la kujifunza maadili kama nidhamu na kujitolea,” amesema.
Sanga ameishukuru serikali ya Dk Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha katika kata yake kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu, afya, maji, umeme, barabara na nyinginezo.
Akizungumzia hali ya maisha ya vijana wengi wakiwemo waliomaliza vyuo vikuu, alisema kilimo kinaweza kuwa chanzo kizuri cha ajira kwa vijana.
“Kupitia miradi ya kilimo, vijana wanaweza kujifunza na kushiriki katika uzalishaji wa chakula na mazao ya biashara, huku wakichangia pia kwenye maendeleo ya kilimo endelevu. Serikali na mashirika yanaweza kusaidia kutoa mafunzo na kutoa rasilimali ili kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika sekta hii ya kilimo,” alisema.