IMF yatabiri uchumi wa Tanzania kuongoza EAC

RIPOTI ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) imesema katika miaka kumi ijayo, uchumi wa Tanzania utakua kwa kasi kuliko Kenya na kuongoza katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Tanzania imeanzisha ushirikiano na nchi na wadau mbalimbali duniani katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na teknolojia, kilimo, madini na ujenzi na hivyo kuifanya kuwa moja ya maeneo bora ya uwekezaji barani Afrika.
Kenya ambayo ni nchi ya kwanza kwa ukuaji wa uchumi EAC, inaweza kubadilika katika miaka 10 ijayo sambamba na kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Kwa mujibu wa ripoti ya IMF, uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa kiwango cha juu zaidi kuliko wa Kenya na kwamba, katika takribani miaka kumi, uchumi wa Tanzania kwa ujumla unaweza kupita wa Kenya.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, matarajio yanaonesha kuwa, ukuaji wa Pato la Taifa kati ya Tanzania na Kenya mwaka 2023 umekuwa asilimia 5.3 kwa Kenya na asilimia 5.2 kwa Tanzania. Mwaka 2024 uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa asilimia 6.4 na Kenya asilimia 5.4. IMF inabainisha kuwa, mwaka 2025 uchumi wa Tanzania utakua kwa asilimia 6.5 na Kenya asilimia 5.5 na mwaka 2026 Tanzania itakuwa na ukuaji wa asilimia 6.8 huku uchumi wa Kenya ukikua kwa asilimia 5.5.
Kuhusu mwaka 2027, uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa asilimia 7 huku wa Kenya ukikua kwa asilimia 5.5. Mwaka 2028 Tanzania itakuwa na uchumi unaokua kwa asilimia 7 na Kenya ukikua kwa kiwango kilekile cha asilimia 5.5. Uchumi wa Tanzania wenye thamani ya Dola bilioni 85.4 kwa sasa, unatabiriwa na IMF kufikia thamani ya Dola bilioni 136 ifikapo mwaka 2028.
Kenya ambayo kwa sasa ina uchumi mkubwa zaidi Afrika Mashariki ikiwa na Dola bilioni 118.1, itakua hadi Pato la Taifa la Dola bilioni 151 ifikapo 2028. Hata hivyo, Tanzania itavuka ukuaji wa uchumi wa Kenya na itakuwa na uchumi mkubwa zaidi katika miaka kumi ijayo kwa kuzingatia mtazamo wa kiuchumi wa IMF na kutumia historia za mataifa hayo mawili katika ukuaji wa pato la taifa.
Kiwango cha maendeleo ya Tanzania kinaweza kuhusishwa na jinsi nchi inavyopokea uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje. Utawala wa sasa wa Tanzania pia unahimiza na hata kuhamasisha uwekezaji wa ndani, kwa ufanisi kuunda mfumo wa ikolojia wa kiuchumi unaofanya uanzishwaji wa mashirika ya kibinafsi na ya umma kuwa mzuri.
Katika miaka michache iliyopita, Tanzania imeshirikiana na mashirika mengi duniani katika nyanja mbalimbali zikiwamo za teknolojia, kilimo, madini na ujenzi. Marekani, Korea Kusini, China na India ni baadhi ya nchi zenye biashara kubwa katika nchi hiyo ya EAC. Kati ya mwaka 2022 na 2023, Tanzania imeshirikiana na nchi kadhaa za Afrika Mashariki, kuondoa ushuru usiofaa wa biashara unaozuia uongezaji wa mapato kwa biashara za ndani.