Bei za vyakula zapandisha mfumuko

MFUMUKO wa bei wa Taifa kwa Februari umeongezeka hadi kufikia asilimia 1.0 kutoka asilimia 0.8 ilivyokuwa Januari mwaka huu.

Aidha, kwa kipimo cha mwaka mfumuko huo kwa Februari umeongezeka hadi asilimia 5.5 kutoka asilimia 5.2 ilivyokuwa Januari mwaka huu.

Kuongezeka kwa mfumuko huo wa bei kunatokana na kupanda kwa bei za bidhaa za vyakula, ambayo imeongezeka hadi asilimia 9.3 kutoka asilimia 8.2 iliyokuwa mwezi januari mwaka huu.

Akizungumza wakati wa kutoa taarifa ya mfumuko wa bei wa Februari, Kaimu Meneja wa Idara ya Takwimu za Ajira na Bei wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ruth Minja alisema, bidhaa za vyakula zilizochangia kuongeza kwa fahirisi za bei ni pamoja na mchele kwa asilimia 4.0, mahindi kwa asilimia 12.2 na unga wa mahindi kwa asilimia 10 pamoja na bidhaa nyingine.