Majaliwa aalika wawekezaji wa Israel

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Israel waje nchini kuwekeza kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo.

Alitoa kauli alipokutana na Balozi wa Israel nchini Tanzania, Yahel Vilan, ofisini kwake bungeni mjini Dodoma.

Waziri Mkuu alisema Tanzania na Israel ni nchi ambazo zina uhusiano mzuri kwa muda mrefu, ambapo ameahidi kwamba serikali itaendelea kuudumisha.

Pia Waziri Mkuu amewakaribisha raia wa Israel kuitembelea Tanzania kama watalii kwa sababu kuna fursa nyingi za utalii ukiwemo mlima wa Kilimanjaro na mbuga nyingi zilizosheheni wanyama.

Kwa upande wake, Balozi Vilan aliipongeza serikali kwa utendaji wake, ambapo amesema viongozi wa kampuni 50 kutoka nchini Israel wanatakuja nchini mwaka huu kushiriki katika jukwaa la biashara na uchumi kati ya Tanzania na Israel.

Alisema mbali na kushiriki katika jukwaa hilo, pia viongozi wa makampuni hayo watapata fursa ya kuangalia maeneo mbalimbali ya uwekezaji nchini.

Pia Balozi Vilan alisema Serikali ya Israel itaimarisha kitendo cha wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa mkoani Dodoma pamoja na kuwajengea uwezo watumishi wa kitengo hicho.