Jukwaa la Biashara Mkoa wa Mwanza: Mkoa wenye fursa lukuki za uwekezaji

JUMANNE ya wiki ijayo, Aprili 11, Mkoa wa Mwanza utakuwa mwenyeji wa Jukwaa la Biashara ambamo mada mbalimbali zitatolewa na wadau wa maendeleo.

Katika jukwaa hilo, washiriki kutoka makundi mbalimbali ya kijamii, wafanyabiashara ndogo na wakubwa, wawekezaji, maofisa wa serikali na wananchi watapata pia nafasi ya kukutana na maofisa wa taasisi muhimu za maendeleo na kuwauliza maswali pamoja na kuanzisha mawasiliano.

Hili ni Jukwaa lililoandaliwa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) inayochapisha magazeti ya Daily News, HabariLeo na SpotiLeo kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. Ni jukwaa linalolenga kutoa elimu ya namna nzuri ya kuziendea fursa za uwekezaji zinazoibuliwa na kuboresha zaidi zilizopo.

Baadhi ya wadau ambao washiriki watapata nafasi ya kusikia mada zinazowasilishwa katika jukwaa hilo na kuwauliza maswali huku wakijenga nao mtandao mpya ni pamoja na; Benki za NMB, TIB (Development), TIB (Corporate) na Benki TPB, Mamlaka ya Mapato (TRA), Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Wengine ni Watumishi Housing Company (WHC), Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI), Mfuko wa Pensheni wa LAPF na Baraza la Biashara Tanzania, Kampuni ya Simu ya nchini (TTCL, Kampuni ya Simu ya Vodacom na Mfuko wa Pensheni wa PPF.

Jana tulianza kuangazia shughuli za kiuchumi mkoani Mwanza kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na tovuti ya mkoa ya www. mwanza.go.tz. Tuliona, japo kwa kifupi, hali ya kilimo na ufugaji vinavyoendeshwa mkoani hapa.

Leo tunaangalia shughuli zaidi za uzalishaji ambazo wadau wake watashiriki kwenye Jukwaa la Biashara na hivyo kujiongezea maarifa zaidi pamoja na maeneo yanayofaa kwa uwekezaji mwingine.

Uvuvi

Uvuvi ni moja ya shughuli kubwa inayofanyika katika Ziwa Victoria. Sekta hii ya uvuvi inachangia asilimia saba ya uchumi wa mkoa kwa mujibu wa tovuti ya mkoa. Inaelezwa kwamba shughuli za uvuvi ndizo zinazoongoza katika kuingiza fedha za kigeni katika mkoa huu. Kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2011, mkoa ulikuwa na jumla ya wavuvi 52,942 huku boti na mitumbwi ikiwa 14,480.

Ufugaji wa samaki

Ufugaji wa samaki imekuwa shughuli mpya inayoanza kuchukua nafasi yake katika siku za hivi karibuni kutokana na kupungua kwa samaki ziwani na hivyo kupunguza pia kipato kwa wavuvi. Hali hii inaelezwa kwamba imesababishwa na uvuvi wa kupita kiasi, uvuvi haramu na usimamizi mbaya wa maji ya Ziwa Victoria.

Kwa kipindi cha miaka minne (2009 - 2011) mkoa ulikuwa na jumla ya mabwawa 128 ya samaki. Ni kwa msingi huo, uwekezaji zaidi katika ufugaji samaki na uvuvi endelevu ni kati ya mambo muhimu yanayohitajika sana kwa sasa.

Mauzo ya samaki

Takribani tani 16,913 za samaki husafirishwa kwenda katika nchi za Umoja wa Ulaya (EU) na nchi za Mashariki ya Mbali za Japan na Australia. Jumla ya tani 426,633.50 za samaki huuzwa katika mikoa mingine ndani ya nchi na takribani tani 6,214.10 hutumika ndani ya Mwanza yenyewe. Kimsingi soko la samaki limekuwa siyo tatizo sana kama upatikanaji.

Maliasili na Utalii

Sekta ya rasilimali za asili nchini inajumuisha ardhi, madini, misitu, ufugaji nyuki, wanyamapori na uvuvi. Tanzania imejaaliwa kuwa na rasilimali nyingi ambazo hazijaendelezwa kwa kiwango kikubwa, hali inayotoa fursa zaidi za uwekezaji katika kuzivuna na mafunzo.

Mbali na ardhi, kuna maeneo yanayofaa kwa utalii, baadhi yakiwa tayari yana wanyamapori na mazingira yanayoweza kutumika kama vivutio vya utalii. Mkoa wa Mwanza pia unayo maeneo mengi yenye vivutio na yanayofaa kuendelezwa kwa ajili hiyo.

Kama ilivyo kwa sekta nyingine, sekta zinazohusu maliasili na utalii, zinahitaji pia uwekezaji zaidi, uwe wa serikali, sekta binafsi au sekta hizi mbili kushirikiana (PPP).

Ukiendelea kufuatilia makala haya katika kipindi chote cha Jukwaa la Biashara linapokuwa mkoani hapa, tutakujuza baadhi ya sekta zilizopo na mipango kambambe ya mkoa wa Mwanza katika kuendeleza sekta ya utalii ambapo sekta binafsi inahitajika sana katika kushirikiana na serikali.

Madini

Sekta ya madini mkoani Mwanza inaelezwa kwamba haijaendelezwa kwa kiwango cha kutosha. Kwa sasa tafiti kadhaa zinaendelea katika kugundua hifadhi za madini, shughuli ambazo zinafanywa na makampuni ya kigeni na ya ndani. Hivi sasa, kuna kiwango kidogo cha uchimbaji madini kinachofanyika katika wilaya za Misungwi, Ilemela na Nyamagana.

Madini yanayovunwa ni dhahabu na yanayohusu shughuli za ujenzi. Madini haya, zaidi hununuliwa na wafanyabiashara katika jiji la Mwanza.

Fursa zaidi za uwekezaji

*Sekta ya afya Mkoa wa Mwanza unaokuwa kwa haraka una fursa za uwekezaji katika ujenzi wa hospitali mpya za kisasa, vituo vya afya na zahanati.

Hali kadhalika, kutakuwa na fursa katika ujenzi wa viwanda vya dawa, maji maalumu yanayotumika kwa ajili ya dripu hospitalini, oksijeni zinatumika kwenye matibabu na vifaa tiba kama vile vitanda na kadhalika. Zinatakiwa pia menejimenti zinazoweza kuendesha hospitali za kisasa na uwekezaji zaidi katika huduma za bima za afya.

Sekta ya elimu

Fursa lukuki pia zipo katika kuanzisha taasisi za elimu na mafunzo katika mkoa wa Mwanza. Mkoa umekuwa ukihimiza sana sekta binafsi kuanzisha shule na vyuo vitakavyotoa mafunzo bora katika fani za menejimenti, sayansi na teknolojia, fedha, masoko na utalii.

Viwanda na Biashara

Katika miaka ya karibuni, sekta ya viwanda na biashara mkoani Mwanza imeonesha kukua kwa kasi ya asilimia 4. Sekta hii kwa sasa ni ya tatu katika kutoa mchango wake kwenye pato la mkoa na ni sekta ya tatu pia katika kuvutia mitaji ya moja kwa moja kutoka nje (FDI) baada ya kilimo na utalii.

Shughuli zinazofanywa na sekta hii ni pamoja na uzalishaji bidhaa za majumbani kama usindikaji wa chakula, vinywaji, nguo na bidhaa zitokanazo na mbao. Mkoa wa Mwanza una uwezo wa kutoa malighafi nyingi na zenye ubora. Malighafi hizo ni zinazotokana na kilimo na mifugo, pia madini na uvuvi.

Kuna fursa kubwa mkoani Mwanza za uanzishwaji wa viwanda vikubwa kama vya kemikali (chemical industries), chakula, vinywaji, nguo, ngozi, metali na kadhalika. Je, kesho nini kitamulikwa katika mkoa wa Mwanza? Fuatilia zaidi.