Mengi awakarimu wafanyabiashara Wafaransa

MWENYEKITI wa kampuni za IPP, Reginald Mengi usiku wa kuamkia jana amewakarimu wageni wafanyabiashara wa Ufaransa waliopo katika wiki ya Ufaransa nchini.

Katika hafla hiyo ya chakula cha usiku iliyofanyika hoteli ya Serena, wafanyabiashara hao wa makampuni makubwa hamsini ya Ufaransa wakiongozwa Balozi wa Ufaransa nchini, Malika Berak walikula huku wakitumbuizwa na mwanamuziki gwiji nchini Zahiri Ally Zoro.

Akizungumza kabla ya kukaribisha wageni wake katika chakula hicho, Mengi amesema kiotendo alichokifanya ni njia mojawapo ya kuonesha shukurani kwa wafanyabiashara hao kwa kuamua kuja nchini kuwekeza.

Alisema: "Jioni hii ya leo sina maneno mengi ya kuzungumza zaidi ya kuwakarimu wageni hawa ambao ni muhimu sana kwa Watanzania, sekta ya uchumi na taifa kwa ujumla."

“Ujio wenu nchini ni wa kufurahisha sana, utatunufaisha taifa na nyie pia; hii ndiyo tunayoita win win situation,” amesema Mengi na kuongeza kuwa ujio wao utasaidia kujenga uwezo wa teknolojia wa taifa hili wakati taifa linaelekea katika uchumi wa viwanda.

Aidha amesema kwa kuwa Ufaransa ni miongoni mwa mataifa yenye msuli wa kiuchumi na kwamba kwa kuwa rafiki wa Tanzania kutasaidia Watanzania kuwa na rafiki mwenye uwezo wa kuwasaidia kuwa na uwezo pia.

Amesema uhusiano wa Tanzania na Ufaransa una historia yake na kwamba kwa sasa utaendelezwa zaidi. Naye Balozi wa Ufaransa nchini, Malika Berak alisema kwamba amefurahishwa sana na ukarimu wa Dk Mengi na kusema kwamba yeye anaamini biashara na urafiki ni kitu muhimu katika kuimarisha mahusiano.

“ …Business and friendship goes together.(biashara na urafiki vinakwenda pamoja).” amesema balozi huyo na kuongeza kwamba kutokana na chakula hicho anaamini kwamba urafiki wa watu wa Ufaransa na Tanzania si wa kubahatisha unakua.