Serikali haijaruhusu vifaranga kutoka nje

HAKUNA mwekezaji yeyote aliyeruhusiwa kupewa kibali cha kuingiza vifaranga au mayai nchini kwa ajili ya biashara, na katika kusimamia hilo kuanzia mwaka 2013 hadi sasa, vifaranga 67,500 vilivyoingizwa nchini kinyume cha sheria viliteketezwa, Bunge limeelezwa.

Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha aliyasema hayo bungeni jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Ukonga Mwita Waitara (Chadema) aliyetaka kujua mpango wa serikali wa kuzuia uingizaji wa mayai kutoka nje kutokana na mayai hayo kuharibu soko la ndani.

Naibu Waziri alisema kuanzia mwaka 2006, serikali iliweka katazo la kuingiza kuku na mazao yake nchini ili kudhibiti ugonjwa hatari wa mafua ya ndege.

Alisema Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Namba 17 ya Mwaka 2003 na Kanuni zake za Mwaka 2007 na 2010 zinatumika kudhibiti na kukagua uingizaji katika maeneo ya mpakani, bandari na viwanja vya ndege.

Alisema serikali inasimamia ubora wa malighafi za kusindika vyakula vya mifugo, kupitia Sheria ya Maeneo ya Nyanda za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Wanyama Namba 13 ya mwaka 2010.

"Changamoto katika kusindika vyakula hivyo, ni gharama kubwa ya viinilishe vya protini kutokana na matumizi ya maharage aina ya soya. Maharage haya huingizwa kutoka nje ya nchi hususani Zambia na India.Wizara inaendelea kuhamasisha uzalishaji wa soya nchini katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini," alisema.

Alisema wako wawekezaji wachache ambao hupewa vibali maalum vya kuingiza nchini mayai au vifaranga vya kuku wazazi tu na kuwa ukaguzi kwa ajili ya kudhibiti uingizaji vifaranga na mayai unaendelea na hatua kali zinachukuliwa kwa yeyote anayekamatwa kwa kukiuka taratibu.