Vyakula soko kuu la Mwanza bei juu

BEI ya vyakula katika soko kuu la Mwanza mjini kwa sasa iko juu kulinganisha na hali ilivyokuwa miezi mitano iliyopita, HabariLeo limegundua.

Uchunguzi uliofanywa gazeti hili jijini Mwanza umegundua kwamba kutokana na kupanda kwa bei, wanunuzi wengi wamepunguza pia kiwango walichokuwa wakinunua kwa ajili ya familia zao.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wenzake, Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko hilo kubwa linalotegemewa na wilaya za Nyamagana na Ilemela, Hamadi Nchola alisema, Novemba mwaka jana kilo moja ya mchele bora ilikuwa ikiuzwa Sh 1,600, lakini sasa inauzwa Sh 2,000.

Chakula kingine kilichopanda alisema kuwa ni mahindi ambapo gunia la kilo 100 linauzwa kati ya Sh 120,000 hadi 130,000 kutoka wastani wa Sh 80,000 mwishoni mwa mwaka jana.

“Mchele ndio chakula kikubwa cha wakazi wa jiji la Mwanza kikifuatiwa na mahindi kwani hata wanaokula ugali wa muhogo wanachanganya na unga wa mahindi. Kwa hiyo vyakula hivyo (mchele na mahindi) vinapopanda bei wananchi wengi wanaumia pia,” alisema.

Alisema kupanda kwa bei ya vyakula pia kunawaumiza wafanyabiashara kwa kuwa wateja wanapungua na mtaji wa kununua bidhaa kwa mfanyabiashara hutakiwa kuwa mkubwa zaidi.

“Wapo pia wateja wanaodhani kwamba sisi tunapandisha bei kwa makusudi kumbe ni kutokana na bei tunayonunulia kutoka kwa wasambazaji wetu,” alisema.

Chakula kingine ambacho kimepanda katika soko hilo na ambacho pia ni chakula kinachokimbiliwa na wengi ni maharage.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti Nchola, maharage yamepanda kutoka wastani wa Sh 1,400 miezi mitano iliyopita kwa kilo hadi kati ya Sh 1,900 na Sh 2,200.

Kwa mujibu wa Nchola, Jiji la Mwanza hupata mchele na mahindi kutoka kwa wakulima wa Mwanza yenyewe, Geita na Shinyanga. Lakini maharage mengi yanatoka Kigoma, Morogoro na Sumbawanga.

“Kilichosababisha bei vyakula kupanda ni ukame ambao umeyakumba maeneo yanayotuletea chakula Mwanza ikiwa ni pamoja na Mwanza yenyewe,” anasema Nchola ambaye amekuwa mfanyabiashara katika soko hilo tangu mwaka 1984.