MSD watoa uhakika wa soko viwanda vya dawa

WAKAZI wa Mwanza wamepewa changamoto ya kuanzisha viwanda vya dawa na vifaa tiba kwa kuwa Bohari ya Dawa (MSD) itawapa soko la uhakika.

Aidha, imeelezwa kwamba ni aibu kuona kwamba hata maji ya dripu ambayo aslimia 95 ni maji ya kawaida, MSD inalazimika kuyaagiza Uganda.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakuni, wakati akizungumza kwenye Jukwaa la Biashara jijini Mwanza.

Jukwaa hilo limeandaliwa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) inayochapisha magazeti ya HabariLeo, Daily News na SpotiLeo, kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

“Mwanza, anzisheni viwanda vya dawa, sisi tutawapatia soko alimradi bidhaa ziwe bora. Ni aibu maji ya dripu, tena yanapita hapa Mwanza, lakini tunayaagiza kutoka nchi jirani ya Uganda... Jamani hata maji tunaagiza?” Alihoji.

Alisema kwamba licha ya mkoa wa Mwanza kulima pamba kwa wingi, lakini vifaa vingi vya hospitalini vinavyotokana na pamba yakiwemo mashuka na bandeji, MSD inaagiza kutoka China.

“Hata gloves ambazo wakati mwingine watu wa saloni wanatuibia tunatoa China,” alisema akionesha masikitiko.

Alisema kwa sasa Tanzania ina viwanda vitano vya kutengeneza dawa lakini bado vinachechemea.

Alisema hata yeye anasikitika kwa jinsi pesa nyingi za kununua dawa na vifaa tiba anavyolazimika kuzipeleka nje wakati zingeweza kubaki ndani kama kungekuwa na viwanda vya kutosha vya dawa.

“Tuna Sh trilioni 1.2 kwa ajili ya kununua dawa kwa mwaka lakini sehemu kubwa zinakwenda nje,” alisema na kufafanua kwamba sehemu kubwa ya pesa hizo zinatolewa na wahisani na sehemu nyingine serikali.

Alisema moja ya dalili za nchi kutoendelea ni kukosa viwanda vya kuzalisha dawa na vifaa tiba.

“Jamani, hata sabuni za kunawa za madaktari tunaagiza.... Angalieni hizo fursa,” alisema.

Awali akizungumza na gazeti hili, alisema dawa zinazotumika sana ni za maumivu, viuavijasimu na sindano ambazo wawekezaji wanapaswa kuzizalisha nchini alimradi ziwe na kiwango bora (mengi tutaandika kwenye makala siku chache zijazo).

Katika hatua nyingine, Bwanakunu alisema kwamvba jana walianza kugawa vitanda 20 kwa kila halmashauri kutokana na zaidi ya Shilingi bilioni 3 zilizotolewa na Rais John Magufuli.

Alisema Rais ametoa vitanda hivyo bure katika kuhakikisha wagonjwa hawalali chini na kwamba halmashauri zote 186 zitapata vitanda hivyo.

Mbali na MSD, wadau wengine walitoa elimu muhimu kwa wafanyabiashara wa Mwanza ni mabenki ya NMB, TIB (Development), TIB (Corporate) na Benki ya TPB.

Taasisi hizi za fedha zilieleza, pamoja na mambo mengine, namna wafanyabiashara wanavyoweza kupata fedha za mitaji alimradi waweze kutekeleza masharti fulani fulani.

Wadau wengine waliotoa mada zao jana ni Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), hoteli ya kisasa jijini Mwanza ya Victoria Palace, Mamlaka ya Mapato (TRA), Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), MSD, na Watumishi Housing Company (WHC).

Pia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) walitazamiwa kutoa mada zao.