Majaliwa ataka tathmini mifuko ya uwezeshaji

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amelitaka Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), lianze kufanya tathmini ya kisayansi kuhusu manufaa ya mifuko yote ya uwekezaji nchini ili kujiridhisha endapo inawanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.

Amelitaka baraza hilo lifanye tathmini kuhusu namna ya kuunganisha mifuko hiyo bila ya kuathiri majukumu ya msingi na mantiki ya kuanzishwa kwake. Alitoa agizo hilo juzi wakati akifungua maonesho ya mifuko ya uwezeshaji katika Uwanja wa Mashujaa mjini Dodoma.

“Lengo ni kuwa na mifuko michache, lakini inayobadilisha maisha ya wanufaika, ambao ni wananchi. Nitafurahi kupata taarifa hiyo kabla au ifikapo Mei, 2018,” alisema. Akaongeza, “Uwezeshaji wananchi kiuchumi ni jambo ambalo lipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/2017- 2020/2021”.

Alisema mifuko hiyo imesaidia upatikanaji wa mitaji kwa wajasiriamali na kupunguza kiwango cha umaskini nchini. “Hadi kufikia mwaka 2016 Mifuko hiyo kwa pamoja ilikuwa imetoa mikopo yenye thamani ya sh trilioni 1.759 kwa wajasiriamali 400,000.

Awali Katibu Mtendaji wa NEEC, Beng Issa alisema kati ya mifuko 19 ya uwezeshaji, mifuko 13 imeweza kushiriki katika maonesho hayo ya kwanza nchini. Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPB Bank PLC, Sabasaba Moshingi alisema kwa niaba ya washiriki wengine kuwa, maonesho hayo yalilenga kukuza uelewa wa watu kuhusu uwepo wa mifuko ya kuwezesha wananchi kiuchumi na fursa zitolewazo na mifuko hiyo.