Tanzanite yaipatia Manyara kodi ya huduma ya mil 20.8/-

SERIKALI kupitia mnada wa madini ya tanzanite imekusanya mrabaha wa dola za Marekani 158,093 sawa na Sh 347,804,600 kati ya hizo, Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara italipwa Sh 20,868,276 kama kodi ya huduma.

Hayo yamebainishwa na Kamishna wa Madini Tanzania, Benjamin Mchwampaka wakati wa kutangaza washindi wa mnada wa madini ya tanzanite katika Maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Madini ya Vito ya Arusha yaliyofanyika jijini humo kuanzia Mei 3 hadi 5, mwaka huu.

Kamishna Mchwampaka alisema madini hayo ya tanzanite yaliyouzwa katika mnada huo yalikuwa ni jumla ya gramu 691,060.33 na kuongeza kuwa, yaliuzwa kwa dola za Marekani 3,161,860 sawa na asilimia 100 ya madini yote yaliyowasilishwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uthaminishaji wa Madini ya Almasi (TANSORT) Wizara ya Nishati na Madini, Archard Kalugendo akitangaza washindi, alizitaja kampuni za Nova Summit International Ltd na Viber Global International Ltd kuwa washindi wa mnada huo.

“Miongoni mwa kampuni zilizoshinda mnada ni pamoja na kampuni ya Kitanzania ya Godi Mwanga and Family Ltd. Hii ni ishara nzuri kwa Tanzania na ninawasihi wadau wengine wa madini nchini kujitokeza. Mnada wa tanzanite ulikuwa wa wazi na aliye bid ( aliyeomba zabuni) kwa kiasi kikubwa ndiye aliyeshinda,” alisema Kalugendo.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini na Maendeleo ya Biashara na Nigeria, Abubakar Bwari aliyeongoza ujumbe wa Serikali ya Nigeria kushiriki maonesho hayo, alitoa pongezi kwa Tanzania kwa kuendelea kudumisha amani iliyopo nchini ikiwemo kupongeza juhudi zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau katika kutangaza madini ya tanzanite pamoja na kuendeleza sekta ya madini.

Akizungumzia sekta ya madini ya Nigeria, alisema hivi sasa nchi hiyo inaweka nguvu katika shughuli za madini na kilimo ili kuhakikisha rasilimali hizo zinalinufaisha taifa hilo.

Aliongeza kuwa imeshiriki maonesho hayo ili kujifunza namna Tanzania inavyoongeza thamani madini yake na kuongeza kuwa, iko tayari kujifunza kutoka Tanzania na kueleza kuwa, hivi karibuni nchi yake itatoa ushindani kwa Tanzania kupitia Maonesho ya Kimataifa ya Vito hususan katika suala la Uthaminishaji wa Madini ya Vito.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo akifunga maonesho hayo aliishukuru Kamati ya Maonesho ya Madini ya Vito ya Arusha (AGF) kwa kuratibu vema zoezi hilo.