Serikali kugawa bure pembejeo za korosho

SERIKALI imetangaza rasmi kugawa pembejeo za korosho bure kuanzia Msimu wa Kilimo wa 2017/2018, ambapo wakulima sasa wapata bure pembejeo aina ya salfa zilizokuwa zikiuzwa kwa bei ya ruzuku.

Kauli hiyo ya Serikali ilitolewa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa anafungua mkutano wa kila mwaka wa wadau wa korosho uliofanyika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Mipango, mjini Dodoma.

Alisema nia ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha vikwazo vyote vilivyokuwa vinawakabili wakulima wa zao hilo vinaondolewa ili kuwawezesha kupata tija zaidi kutokana na zao lao.

“Mheshimiwa waziri wa kilimo mifugo na uvuvi, hebu sema lile tuliloazimia kuhusu pembejeo kuanzia msimu wa mwaka huu… tunataka wajumbe wa mkutano huu muhimu wajue nini sisi kama serikali tumekubaliana”, alisema Majaliwa huku akimwinua waziri huyo kutoa kauli ya serikali kwa niaba yake.

Alisema lengo la Serikali ni kuona mashamba yaliyotelekezwa na yenye mikorosho iliyozeeka yanafufuliwa ili kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi wa wakulima na nchi kujipatia kipato cha kutosha.

“Mikorosho asilimia 25 iliyopo sasa ni ile iliyozeeka ambayo haizalishi kiasi cha kuridhisha…lakini pia kuna mashamba yaliyotelekezwa kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukosa mitaji kwa ajili ya kununua pembejeo,hivyo basi kwa hatua hii tunatarajia yatafufuliwa”, alisema Majaliwa huku akishangiliwa na wadau hao.

Awali akitoa taarifa kwa mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Nchini (CBT), Anna Abdallah, alisema bodi hiyo imenunua tani 18,000 za pembejeo aina ya Salfa ambayo inatumika kudhibiti na kutibu ugonjwa wa ubwiriunga unaowasumbua wakulima wa zao hilo.

Alisema kiasi hicho ni sawa na asilimia 95 ya pembejeo zote zilizoagizwa kwa msimu huu wa kilimo, ambapo pembejeo nyingine ni pamoja na dawa za maji za kunyunyizia na mabomba ya kupulizia na jumla ya Sh bilioni 43.5 zitatumika katika kununua, kusambaza na malipo ya mawakala.

“Mwaka huu tutafikisha pembejeo za ruzuku hadi wilayani badala ya ule mfumo wa miaka yote wa kuwa na vituo vichache…na tayari tumeshapokea pembejeo zote tunasubiri muda muafaka tuanze kusambaza kwa wakulima,” alisema Anna.

Akitoa taarifa za mapato yatokanayo na mazao ya biashara, Waziri wa Kilimo, Uvuvi na Ushirika, Dk Charles Tizeba alisema korosho imeongoza kwa kuliingizia taifa fedha za kigeni kutokana na mauzo ya zao hilo nje ya nchi katika msimu uliopita.

Tizeba alisema jumla ya dola za kimarekani milioni 300.46 (sh bilioni 630.9)n zilipatikana kutokana na mauzo hayo na hivyo kuongoza na kufuatiwa na zao la tumbaku, katika msimu huo tani 260,000 zilikusanywa na kuuzwa kwa mnada kwa wanunuzi wa ndani na nje ya nchi.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amewaonya watendaji wa serikali na viongozi wa vyama vya ushirika wanaoshirikiana na wafanyabiashara wasio waaminifu kununua korosho nje ya mfumo wa ununuzi wa stakabadhi ghalani (kangomba) na kwamba ikibainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Alisema serikali kuanzia msimu uliopita imefanya mazungumzo na wanunuzi wakubwa kutoka nchi mbalimbali ili kuja nchini kununua korosho badala ya kutegemea wafanyabiashara kutoka India pekee kama ilivyozoeleka na matokeo ni kupanda kwa bei ambapo ilifikia hadi Sh 4,000 kwa kilo.