Serikali kuongeza uwekezaji wa trilioni 5/-

SERIKALI imesema imejipanga kuhakikisha inaongeza uwekezaji wa Sh trilioni tano katika viwanda kwa mwaka, kwa kuhakikisha inaweka mazingira mazuri ya uwekezaji hali itakayoindoa Tanzania kwenye aibu ya kuagiza hadi bidhaa ndogo kutoka nje ya nchi. Hata hivyo, imesisitiza kuwa mpaka sasa nchi hiyo inafanya vizuri katika kuvutia uwekezaji kwani kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2007, Tanzania ilishika nafasi ya 132 kutoka 144 kati ya 190 kwa kuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji.

Akijumuisha mjadala wa wabunge wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Waziri wa wizara hiyo, Charles Mwijage alisema akiwa kama waziri wa viwanda atahakikisha uwekezaji wa viwanda unapanda zaidi ya uwekezaji wenye thamani ya trilioni tano wa mwaka jana.

Alikiri kuwa pamoja na sekta ya viwanda kwa sasa kuanza kufanya vizuri bado kuna haja ya kuhakikisha uwekezaji unaongezeka na kuanzisha viwanda mbalimbali muhimu vikiwemo vya madawa.

Mwijage alisema serikali imejipanga kuhakikisha inashughulikia vikwazo vyote vinavyowakabili kwa sasa wawekezaji ikiwa ni pamoja na kutumia maoni ya wabunge na wadau juu ya namna ya kuboresha zaidi uwekezaji nchini.

Alikiri kuwa kuwapata wawekezaji ni shida hivyo ni vyema wakatengenezewa mazingira mazuri katika nyanja zote kwani, endapo watakwazika watakimbilia nchi nyingine na matokeo yake Tanzania inaweza kugeuzwa soko.