Stakabadhi ghalani kutumika zao la mbaazi

WIZARA inaangalia uwezekano wa kuanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani kwenye zao la mbaazi ambao umeleta matokeo mazuri kwenye zao la korosho.

Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na uvuvi, William Ole Nasha alieleza mkakati huo wakati akijibu swali la Mbunge wa Karatu, Qambalo Qulwi (Chadema) aliyetaka kujua serikali ina mpango gani wa kuunganisha wakulima wa zao hilo na masoko yaliyo ndani na nje ya nchi ili wapate bei nzuri.

Nasha alisema, mfumo huo wa stakabadhi ghalani umeleta matokeo mazuri kwa zao la korosho, hivyo vema pia ukitumika kwa zao la mbaazi. Katika kuhakikisha mfumo huo unaleta ufanisi, Serikali itawahamasisha wakulima kujiunga katika vyama vya ushirika kwenye maeneo yao na pia, kuwa na utaratibu wa kupanga bei elekezi inayozingatia gharama za uzalishaji kama ilivyo kwa zao la korosho.

Nasha alisema ili kuhakikisha wakulima wanapata soko la uhakika la mbaazi, Serikali kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko iliandaa mkataba wa makubaliano na Serikali ya India.

Alisema mkataba huo ulipelekewa India ambako kwa mujibu wa Ubalozi wa India nchini, bado wanaufanyia kazi kabla ya kusainiwa na pande zote mbili. Nasha alisema bei ya mbaazi iliporomoka katika msimu wa 2016/17 kutokana na ongezeko la uzalishaji wa zao hilo China, Brazil, Mnyanmar, Canada, Msumbiji na Sudan.