‘Uchumi Tanzania unakua kwa kasi barani Afrika’

BALOZI mdogo wa Ujerumani nchini, John Reyes amesema Tanzania ni miongoni mwa mataifa yanayokua kwa kasi kiuchumi katika Bara la Afrika hivyo kuvutia wawekezaji wengi kutokana na mazingira mazuri ya biashara.

Akizungumza nyumbani kwake jana katika hafla ya kupongeza kampuni zinazotangaza bidhaa za Kijerumani katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba, Balozi Reyes alisema nchi yake inatazamia kuwekeza zaidi katika ardhi ya Tanzania. “Kwa mara nyingine, Ujerumani inapeperusha bendera yake katika Maonesho ya Sabasaba, hii ni ishara nzuri kuwa sehemu ya wawekezaji kwenye taifa linalokua kwa kasi kiuchumi. Katika Afrika Mahsariki na Kati pamoja na Afrika nzima Tanzania imeonesha kukua kwa kasi.

“Kuna fursa nyingi za uwekezaji na ndiyo maana bidhaa kutoka Ujerumani zimekuwa zikiongezeka. Kampuni ya CFAO Motors inayouza magari yakiwamo Volkswagen na Mercedes Benz kutoka Ujerumani ni miongoni mwa kampuni zitakazoshiriki maonesho haya, nwaomba mfike kwenye banda letu la Ujerumani muone bidhaa nyingi zaidi,” alisema Balozi Reyes.

Alisisitiza kuwa amani na nia ya dhati ya kukua kiuchumi ni miongoni mwa tunu zinazoifanya Tanzania kutazamwa kwa jicho zuri na mataifa yaliyoendelea kiviwanda. Hivyo atatumia nafasi yake kuhakikisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, kuwa na uchumi wa kati na viwanda ifikapo mwaka 2025, inatimia kwa kiasi kikubwa. Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko CFAO Motors, Tharaia Ahmed akiwa katika ghafla hiyo, alisema kampuni yao imekuwepo nchini tangu mwaka 1952 wakati huo ikiitwa DT Dobie, maana yake wanalitambua soko la Tanzania vizuri.

“Magari tunayoingiza nchini ni yale yaliyotengenezwa kutokana na mazingira ya kitanzania, tumekuwepo Tanzania tangu enzi za Tanganyika kwa zaidi ya miaka sitini tunahudumia watanzania. Tunajua huu ni ukanda wa vumbi hivyo tunaagiza magari yenye vifaa vya kuzua vumbi kuharibu gari pamoja na aina ya barabara zilizopo magari yetu yanastahamili,” alisema Ahmed.

Alibainisha kuwa watu wasiangalie gharama, bali waangalie uwekezaji katika vyombo vya usafiri vinavyodumu na kustahimili mazingira magumu. Kwa upande wake, mmoja wa wafanyabiashara mwenye asili ya Ujerumani anayeishi nchini, Bob Hooda kutoka Kampuni ya WIPRO alisema kwa sasa Tanzania inaingia katika uchumi wa viwanda hivyo itahitaji umeme wa uhakika, miongoni mwa shughuli wanazofanya zinahusiana na umeme.