Mhagama aipongeza kampuni kwa uwekezaji

WAZIRI wa Nchi, Ofi si ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama ameipongeza kampuni ya Matomondo One kwa kuwekeza katika miradi itakayoinua kipato cha wakulima na wafugaji wa Mkoa wa Ruvuma na jirani zake.

Alitoa pongezi hizo wakati akikagua mradi wa kampuni hiyo katika Kijiji cha Matomondo wilayani Songea mkoani Ruvuma. Kampuni hiyo ina miradi ya kufuga kuku na nguruwe na imeanza kujenga maghala makubwa kwa ajili ya kiwanda cha kusindika mafuta.

Alimshukuru Mkurugenzi wa Matomondo One, Daniel Msembele kwa kujitoa na kuanzisha miradi hiyo itakayoongeza ajira kwa wananchi wa maeneo hayo na kuinua uhitaji wa malighafi inayotoka kwa wakulima, na itachochea ukuaji wa soko kati ya mataifa ya Msumbiji na Tanzania kwa kuwa wapo karibu na mpaka.

Waziri Mhagama aliitaka Halmashauri ya Songea Vijijini kuwa karibu na wawekezaji wanaojitokeza kuweka viwanda kwa kuwapa na kuwasaidia kufanikisha miradi hiyo. Akizungumzia haja ya wananchi wengi kujiunga na kuanzisha vitega uchumi, alisema nchini kuna fursa za mifuko 18 ambayo inatoa mikopo kwa masharti nafuu inayoweza kusaidia kuimarisha uwekezaji hasa kwa kutumia mali ghafi zinazopatikana maeneo husika.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Songea Vijijini, Rajabu Mtiula amemuahidi Mkurugenzi wa Matomondo One kushirikiana naye katika kuboresha kiwanda cha usindikaji nafaka na mafuta na kuboresha mradi wa ufugaji na kilimo.

Mwakilishi wa Matomondo One, Catherine Msembele katika taarifa ya mradi huo, alisema shabaha ya kuanzisha Matomondo One ni kusaga na kusindika nafaka ya mahindi na kukamua mafua ya alizeti.

Aidha, katika mradi wake wa kilimo wamepania kuwezesha uwapo wa uhakika wa pembejeo za kilimo, nguruwe na vifaranga vya kuku. Alisema pamoja na kuhakikisha uwapo wa bidhaa hizo pia wamepania kutoa elimu ya kilimo na ufugaji kwa wananchi wanaozunguka Matomondo One na kuhamasisha vijana kujihusisha na kilimo.