Benki ya TPB ilivyodhamiria kuinua wenye kipato kidogo

SERIKALI ya awamu ya tano imedhamiria kuboresha maisha ya Watanzania kupitia huduma mbalimbali kuelekea Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati. Uwapo wa taasisi za fedha za kutosha na zenye uwezo na weledi, ni nyenzo muhimu ya kufanikisha azma hiyo.

TPB PLC ni taasisi ya umma inatajwa kukua na kuhimili ushindani katika utoaji huduma za kibenki kwa kufikia wananchi wengi hususani wa kipato cha kawaida. Wakati Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Sabasaba Moshingi akiainisha maeneo mbalimbali yanayodhihirisha kukua kwake, uchangiaji mapato katika hazina kuu ya serikali, ni hatua ambayo imeiweka katika nafasi nzuri kimapato.

Mathalani, hivi karibuni imechangia mapato Hazina kuu ya serikali kwa kutoa gawio la Sh bilioni 1.032 kwa serikali ambaye ni mwekezaji mkuu mwenye hisa asilimia 86.17. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango anaeleza kuridhishwa na hatua hiyo.

Anaipongeza benki hiyo kwa gawio hilo na kwa kile anachoeleza kuwa, ni kufanya kazi kwa weledi. “Dhamira ya serikali ni kuwawezesha kiuchumi wananchi wa kipato cha chini, nafarijika kuona ninyi mnaifanya kazi hiyo vizuri,” anasema waziri wakati akipokea hundi ya gawio hilo, hivi karibuni mjini Dodoma.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Moshingi, anaelezea zaidi safari ya benki hiyo kibiashara tangu ilipoanzishwa hadi sasa huku akisisitiza kuwa, kama ilivyo kwa taasisi yoyote ya umma, imejikita kuwafikia watanzania wote bila kujali vipato vyao.

Benki hii ilianzishwa na Sheria ya Bunge Na. 11 ya mwaka 1991 na kufanyiwa marekebisho mwaka 1992, ikijulikana kwa jina la TPB. Kutokana na Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 kuzitaka benki zote nchini kuanzishwa chini ya sheria ya Makampuni Sura Namba 212 au sheria ya vyama vya ushirika sura namba 211, mwaka jana TPB ilikwenda kwa msajili na kujisajili kwa matakwa ya sheria hiyo na kuanza kujulikana kama TPB PLC.

Anasema wameweza kutoa gawio kwa serikali na kwa wanahisa wengine ambao ni Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (hisa 3.05), Shirika la Posta Tanzania (hisa 7.98) na TP &TC Saccos (hisa 2.79).

Benki hii iliyoanzishwa na Sheria ya Bunge Na 11 ya mwaka 1991 na kufanyiwa marekebisho mwaka 1992, kwa mujibu wa Moshingi, asilimia 70 ya wateja wao ni wenye kipato cha wastani na wale wenye kipato kidogo.

Anasema ingawa mtazamo wa benki yake ni kuhudumia Watanzania wote, lakini umuhimu umewekwa kwa wenye kipato cha chini. Katika kutekeleza jukumu hilo, wamekuwa wakitoa huduma za mikopo kwa wateja hao katika vikundi vyao vya biashara na hata kwa mteja mmoja mmoja.

Anasema unafuu wa gharama za uendeshaji akaunti pia ni kivutio cha wateja wengi wenye kipato cha chini. Anaeleza siri ya kukua kwao kuwa ni kuwa karibu na wateja. Kwa mujibu wa Moshingi, matawi ya benki hiyo yameongezeka kutoka 33 hadi 60 nchini.

“Matawi hayo yaliyoongezeka yamesambaa kote nchini yakilenga kuwafikia Watanzania wote wa kipato cha chini na cha juu,” anasema. Katika miaka mitano iliyopita hadi mwaka huu wa fedha, benki hiyo inaendelea kuainisha mafanikio yake ikisema mapato yameongezeka kutoka Sh bilioni 20 kwa mwaka 2010 hadi kufikia Sh bilioni 92 kwa mwaka jana.

Faida kabla ya kodi imekua kutoka Sh milioni 900 kwa mwaka 2010 hadi kufikia Sh bilioni 15.7 kwa mwaka jana. Aidha, katika kipindi hicho, amana imeongeze kutoka Sh bilioni 109 hadi Sh bilioni 337; utoaji wa mikopo umetoka Sh bilioni 65 hadi Sh bilioni 298. Mtaji wa benki pia umeongezeka kutoka Sh bilioni 7.7 mwaka 2010 hadi Sh bilioni 51.8 mwaka jana.

Kuongezeka kwa matawi ni jambo ambalo anasisitiza kuwa ni la mafanikio makubwa kwa benki yoyote. Katika miaka sita iliyopita, matawi makubwa yalikuwa 28 na madogo yalikuwa matano lakini sasa, makubwa yamefika 30 na madogo ni 30.

Akielezea kuridhishwa na mwamko wa Watanzania katika matumizi ya mashine za kutolea fedha (ATM), anasema benki yake imeongeza na sasa yamefikia 48 . “Mafanikio hayo yote, ni uthibitisho tosha kwamba benki yetu inaweza kukua na kushindana na zile za sekta binafsi na kufuta dhana kwamba taasisi za umma haziwezi kukua na kishindana,” anasema.

Matarajio ya benki hiyo ni kuendelea kutoa huduma ikiwamo mikopo kwa wananchi hasa wale wa kipato cha chini ili kukuza kipato chao. Anasema hatua hiyo ina mchango mkubwa katika kuipeleka nchi kwenye uchumi wa kati.

Anatoa mwito kwa Watanzania hasa wale wa kipato cha chini kuendelea kujiunga na benki yake ili waweze kupata huduma bora kwa gharama nafuu, huduma ambazo anasema zitasaidia kukuza kipato chao. Beatus John, ni mkazi wa Ilala, Dar es Salaam ambaye anatoa mwito kwa taasisi zote za fedha kuwa karibu na wateja hususani wa kipato cha kawaida.

“Namaanisha wawe karibu na sisi watu wa kipato cha kawaida kwa kutuletea huduma karibu lakini pia na kutupatia mikopo ya kutuinua kiuchumi,” anasema John ambaye anakiri kunufaika na mkopo alioupata katika benki hiyo ya TPB.