CRDB yatakiwa kuondoa msongamano

RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, amesema miongoni mwa changamoto zinazowakabili wateja wa benki nyingi hapa nchini ni msongamano wa wateja pamoja na ucheleweshaji huduma na ameitaka Benki ya CRDB kuwa na mikakati katika kupambana na kadhia hiyo.

Alisema hayo jana Chake Chake, Pemba katika sherehe ya ufunguzi wa tawi jipya la Benki ya CRDB likiwa tawi la 280 ndani ya mtandao wa benki hiyo kutoka matawi 19 iliyokuwa nayo mara baada ya kuanzishwa mnamo mwaka 1996.

Alisema ameelezwa na wananchi kuwa, miongoni mwa changamoto zinazosababisha msongamano ni kuwa benki za nchini bado haziendani na kasi ya mabadiliko yanayotokea katika sekta ya fedha.

Aliongeza kuwa, katika Siku ya Sherehe za Maadhimisho ya Mei Mosi, mwaka huu yaliyofanyika katika viwanja vya Mahonda, Unguja, wafanyakazi walipendekeza Serikali ikae na uongozi wa benki mbalimbali ili ione namna ya kupunguza kero hiyo kubwa ya msongamano na kuchelewa kutolewa huduma, hasa ifikapo mwisho wa mwezi.

“Leo nimeona ni busara nikuleteeni mawazo hayo ya wafanyakazi, ambao pia, ni baadhi ya wateja wa benki zenu. Wahenga wanasema ‘Mjumbe hauawi’ ndio maana na mimi nimeufikisha ujumbe kama nilivyoambiwa”, alisema Dk Shein.