Majaliwa azifagilia NSSF, PPF kwa uwekezaji

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa (pichani) amepongeza hatua ya mifuko ya hifadhi ya jamii nchini kuwekeza kwenye sekta ya viwanda huku akitoa mwito kwa jamii hususani vijana kuhakikisha wanaonesha uzalendo kwa kujitolea kwa vitendo kuunga mkono jitihada hizo zinazolenga kutatua tatizo la ajira na kuinua uchumi wa taifa.

Majaliwa alitoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki mkoani hapa baada ya kuongoza upandaji wa miwa ikiwa ni ishara ya kuunga mkono mradi mkubwa wa ujenzi wa kiwanda cha sukari unaofahamika kama Mkulazi II, unaotekelezwa kwa ubia kati ya mifuko ya hifadhi ya jamii ya NSSF na PPF kupitia Kampuni Hodhi ya Mkulazi Holding unaofanyika katika Gereza la Mbigiri, Dakawa wilayani Mvomero mkoani Morogoro.

“Pamoja na kutoa pongezi kwa mifuko yetu ya hifadhi ya jamii hapa nchini kwa kuitikia vema wito wa Serikali ya Awamu ya Tano katika uwekezaji wa viwanda vyenye tija kwa taifa, kipekee nitoe wito kwa jamii hususani vijana kuhakikisha wanaunga mkono jitihada hizi kwa kujitolea ujuzi na maarifa katika kufanikisha azma hii ya serikali inayolenga kuwanasua kutoka kwenye uhaba wa ajira,” alieleza