Bil. 30.6/- zapatikana mnada wa almasi

JUMLA ya Sh bilioni 30.6 kimepatikana katika mnada wa tatu wa mauzo ya almasi kutoka mgodi wa Mwadui mkoani Shinyanga. Hatua hiyo itaiwezesha serikali kuvuna kiasi cha zaidi ya Sh bilioni mbili kutokana na ada ya ukaguzi pamoja na mrabaha.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema leo jijini Dar es Salaam kuwa, mauzo ya almasi hizo kutoka kampuni ya uchimbaji madini ya ‘Williamson Diamond Limited’ yalifanyika nchini Ubelgiji kati ya Februari 2 hadi 9 mwaka huu na kuhudhuriwa na baadhi ya maofisa kutoka wizara hiyo.

Amesema, katika mnada huo, jumla ya Karati 54,094.47 ziliuzwa, ambapo kampuni 145 zilishiriki katika mnada huo na kuwasilisha zabuni zao za ununuzi zipatazo 1,019, idadi hiyo ni nyingi kushinda zingine zilizowahi kuwasilishwa katika minada miwili ya awali.

“Mrabaha wa awali uliolipwa kutokana na uthaminishaji kabla ya mauzo pamoja na ada ya ukaguzi, umeiwezesha Serikali kupata kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 1.7 kutokana na madini hayo, na hivyo kuchangia uchumi wa nchi yetu,” amesema Biteko.

Mbali na hatua hizo, Serikali inatarajia kuanzisha utaratibu wa kufanya minada ya madini hayo na mengineyo hapa nchini ili kujiongezea wigo wa upatikanaji wa fedha za kigeni na kuitangaza Tanzania katika mataifa mengine.

Amesema, uanzishwaji wa mnada huo kwa sasa, upo katika mchakato mzuri, huku akiamini kuwa kuanzishwa kwa utaratibu huo, utaliingizia taifa fedha za kigeni na kuitangaza kimataifa, pia itasaidia kukuza utalii wa nchi yetu.

Biteko amewataka wananchi na wadau wa sekta ya madini, wenye nia ya kutaka kusafirisha madini kwenda nje ya nchi, kuomba vibali vya usafirishaji wa madini hayo katika Tume ya Madini.

Amesema utaratibu huo unatokana na marekebisho ya Sheria za Madini za mwaka 2017 na kusainiwa kwa Kanuni za Madini za mwaka 2018 na Waziri wa Madini, inayotaka vibali hivyo kusainiwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini.

Biteko amesema vibali hivyo vitaombwa kuanzia ngazi ya mkoa, hivyo kuwataka wadau wote wa sekta ya madini kuzingatia utaratibu huo ili kuepukana na usuambufu usio na tija.

Katika hatua nyingine, serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), wataanza usajili wa vitambulisho kwa wachimbaji wa madini waliopo eneo la Mererani. Lengo la hatua hiyo ni kudhibiti wachimbaji wasio wazawa kuingia katika mgodi huo, hatua itakayosaidia pia ulinzi wa madini hayo ya tanzanite.

Amesema, uandikishwaji wa vitambulisho hivyo, unatarajiwa kuanza Jumatatu ijayo hivyo kutoa fursa kwa wachimbaji hao na wananchi wengine kutoka wilaya ya Simanjiro, kupatiwa vitambulisho, vitakavyowasaidia katika shughuli mbalimbali.