Wauza nyama wailalamikia TRA

CHAMA cha Wauzaji wa Nyama katika Jiji la Arusha (Wanjamuco) kimelalamikia Mamlaka ya Mapato (TRA) mkoani hapa kwa kupandisha kodi ya mapato kutoka Sh 318,000 hadi Sh milioni moja kwa mwaka.

Walisema hayo katika kikao cha pamoja kilichoketi katika machinjio ya Jiji la Arusha wakati wakipatiwa elimu ya matumizi sahihi ya mashine za kielektroniki (EFDs) na umuhimu wa kulipa kodi.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Alex Lasiki, alisema kiwango hicho ni kikubwa na kinawaumiza hasa ikizingatiwa wametakiwa kuanza kutumia EFDs wakati wa mauzo ya nyama kwa kila bucha na kwamba Februari 14, mwaka huu ilikuwa ni siku ya mwisho kufanya biashara hiyo bila kuwa na mashine hizo.

Wameiomba TRA kuangalia uwezekano wa kuwapunguzia kiwango hicho cha kodi na kufikia walau Sh 600,000, wakidai biashara ya nyama ni ya kubahatisha na nyama huwa inapungua uzito kila wakati.

“Unajua kiwango tulichopewa kulipa cha shilingi milioni moja ni kikubwa sana, maana hii biashara yetu ya nyama tunanunua ng’ombe kwa kumkadiria uzito na mara nyingi, unapoenda kupima kwenye mizani baada ya kumchinja unakuta kilo sio zenyewe na hivyo unapata hasara,” alisema Lasiki.

Wafanyabiashara Richard Mboya, Medeus Massawe, Humphrey Minja, walisema biashara ya nyama wanaifanya kwa makadirio na wanapochinja ng’ombe kiasi fulani cha uzito hupotea na kuwasababishia hasara.

Wameishauri serikali kuangalia upya utaratibu wa kuuza ng’ombe kwa kutumia mizani ili kuondoa ukadiriaji ambao baadaye umekuwa ukiwapatia hasara pindi wanapoenda kuchinja ng’ombe.

Ofisa Kodi wa TRA Mkoa wa Arusha, Marliseri aliwaeleza wafanyabiashara hao taratibu za mabadiliko ya kodi akisema, mfanyabiashara mwenye mtaji wa kuanzia Sh milioni 7.5 hadi milioni 11.5, atapaswa kulipa kodi ya Sh 318,000 kwa mwaka.

Aidha, alisema mfanyabiashara mwenye mtaji wa Sh milioni 11.5 hadi Sh milioni 16, atapaswa kulipa Sh 546,000 kwa mwaka na mwenye mtaji wa Sh milioni 16 hadi 20 atapaswa kulipa Sh 862,000 kwa mwaka.