SMZ yahitaji ndege za ATCL Pemba

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imeanza mazungumzo na uongozi wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kuhusu uwezekano wa kutoa huduma za safari za anga katika kisiwa cha Pemba.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Mohamed Ahmada wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Chakechake, Suleiman Sarhani aliyetaka kujua kwa nini hadi sasa ATCL ambayo ni taasisi ya muungano imeshindwa kufanya safari zake katika kisiwa cha Pemba na kulipatia ufumbuzi tatizo la usafiri linalowakabili wananchi.

Akitoa ufafanuzi zaidi, Ahmada alisema katika hatua za awali wamefanya mazungumzo na uongozi huo kuhusu kufanya safari katika kisiwa cha Pemba.

Alisema ni kweli huduma nyingi zimeimarika katika kisiwa cha Pemba ikiwemo sekta ya utalii na biashara ambapo suala la kuwepo kwa huduma za ndege za uhakika zinahitajika.

''Tumefanya mazungumzo na uongozi wa ATCL kuhusu kufanya safari katika kisiwa cha Pemba ambapo suala hilo wamesema wanalichukua na kulifanyia utafiti kupitia kitengo chao cha biashara,” alisema.

Alisema ili kufanya safari za ndege za Pemba suala la utafiti linahitajika kuona kwamba kampuni inafanya biashara yenye tija na sio kuingia hasara. Hata hivyo, Ahmada alisema tayari yapo mashirika mbalimbali ya binafsi yanayofanya safari katika kisiwa cha Pemba ambapo milango ipo wazi.